Marko 10
Swahili NT
1Yesu alitoka hapo akaenda mkoani Yudea na hata ng'ambo ya mto Yordani. Umati wa watu ukamwendea tena, naye akawafundisha tena kama ilivyokuwa desturi yake.

2Basi, Mafarisayo wakamwendea, na kwa kumjaribu wakamwuliza, "Je, ni halali mtu kumpa talaka mkewe?" 3Yesu akawajibu, "Mose aliwapa maagizo gani?" 4Nao wakasema, "Mose aliagiza mume kumpatia mkewe hati ya talaka na kumwacha." 5Yesu akawaambia, "Mose aliwaandikia amri hiyo kwa sababu ya ugumu wa mioyo yenu. 6Lakini tangu kuumbwa ulimwengu, Mungu aliumba mwanamume na mwanamke. 7Hivyo mwanamume atawaacha baba yake na mama yake, ataungana na mkewe, 8nao wawili watakuwa mwili mmoja. Kwa hiyo, wao si wawili tena bali mwili mmoja. 9Basi, alichounganisha Mungu, binadamu asitenganishe."

10Walipoingia tena ndani ya nyumba, wanafunzi wake walimwuliza juu ya jambo hilo. 11Naye akawaambia, "Anayemwacha mkewe na kuoa mwingine, anazini dhidi ya mkewe. 12Na mwanamke anayemwacha mumewe na kuolewa na mwingine anazini."

13Watu walimletea Yesu watoto wadogo ili awaguse, lakini wanafunzi wakawakemea. 14Yesu alipoona hivyo, alikasirika akawaambia, "Waacheni hao watoto waje kwangu, wala msiwazuie, kwa maana Ufalme wa Mungu ni kwa ajili ya watu walio kama watoto hawa. 15Nawaambieni kweli, mtu yeyote asiyeupokea Ufalme wa Mungu kama mtoto mdogo hataingia katika Ufalme huo." 16Kisha akawapokea watoto hao, akawawekea mikono, akawabariki.

17Yesu alipoanza tena safari yake, mtu mmoja alimjia mbio, akapiga magoti mbele yake, akamwuliza, "Mwalimu mwema, nifanyeje ili niupate uzima wa milele?" 18Yesu akamjibu, "Mbona unaniita mwema? Hakuna aliye mwema ila Mungu peke yake. 19Unazijua amri: Usizini; Usiue; Usiibe; Usitoe ushahidi wa uongo; Usidanganye; Waheshimu baba na mama yako." 20Naye akamjibu, "Mwalimu, hayo yote nimeyazingatia tangu ujana wangu." 21Yesu akamtazama, akampenda, akamwambia, "Umepungukiwa na kitu kimoja: nenda ukauze vitu ulivyo navyo, uwape maskini, nawe utakuwa na hazina mbinguni; kisha njoo unifuate." 22Aliposikia hayo, alisikitika, akaenda zake akiwa na huzuni, kwa maana alikuwa na mali nyingi.

23Yesu akatazama pande zote, akawaambia wanafunzi wake, "Jinsi gani itakavyokuwa vigumu kwa matajiri kuingia katika Ufalme wa Mungu!" 24Wanafunzi walishangazwa na maneno yake. Yesu akawaambia tena, "Watoto wangu, ni vigumu sana kuingia katika Ufalme wa Mungu! 25Ni rahisi zaidi ngamia kupenya katika tundu la sindano, kuliko tajiri kuingia katika Ufalme wa Mungu." 26Wanafunzi wake wakashangaa sana wakaulizana, "Ni nani basi, atakayeweza kuokoka?" 27Yesu akawatazama, akawaambia, "Kwa binadamu haiwezekani, lakini kwa Mungu si hivyo, maana kwa Mungu mambo yote huwezekana."

28Petro akamwambia, "Na sisi je? Tumeacha yote, tukakufuata!" 29Yesu akasema, "Kweli nawaambieni, kila mtu aliyeacha nyumba, au ndugu, au dada, au mama, au baba, au watoto au mashamba kwa ajili yangu na kwa ajili ya Habari Njema, 30atapokea mara mia zaidi wakati huu wa sasa nyumba, ndugu, dada, mama, watoto na mashamba pamoja na mateso; na katika wakati ujao atapokea uzima wa milele. 31Lakini wengi walio wa kwanza watakuwa wa mwisho, na walio wa mwisho watakuwa wa kwanza."

32Basi, walikuwa njiani kwenda Yerusalemu, na Yesu alikuwa anawatangulia. Wanafunzi wake walijawa na hofu, na watu waliofuata waliogopa. Yesu akawachukua tena kando wale kumi na wawili, akaanza kuwaambia yale yatakayompata: 33Sikilizeni! Tunakwenda Yerusalemu, na huko Mwana wa Mtu atakabidhiwa kwa makuhani wakuu na walimu wa Sheria, nao watamhukumu auawe na kumkabidhi kwa watu wa mataifa. 34Nao watamdhihaki; watamtemea mate, watampiga mijeledi na kumwua. Na baada ya siku tatu atafufuka."

35Yakobo na Yohane, wana wa Zebedayo, walimwendea Yesu wakamwambia, "Mwalimu, tunataka utufanyie kitu tutakachokuomba." 36Yesu akawauliza, "Mnataka niwafanyie nini?" 37Wakamjibu, "Uturuhusu tuketi mmoja upande wako wa kulia na mwingine upande wako wa kushoto katika utukufu wa Ufalme wako." 38Yesu akawaambia, "Hamjui mnachoomba! Je, mnaweza kunywa kikombe nitakachokunywa, au kubatizwa kama nitakavyobatizwa?" 39Wakamjibu, "Tunaweza." Yesu akawaambia, "Kikombe nitakachokunywa mtakinywa kweli, na mtabatizwa kama nitakavyobatizwa. 40Lakini ni nani atakayeketi kulia au kushoto kwangu si wajibu wangu kupanga, bali nafasi hizo watapewa wale waliotayarishiwa."

41Wale wanafunzi wengine kumi waliposikia hayo, walianza kuchukizwa na Yakobo na Yohane. 42Yesu akawaita, akawaambia, "Mnajua kwamba wale wanaofikiriwa kuwa watawala wa mataifa huwatawala watu wao kwa mabavu, na wakuu hao huwamiliki watu wao. 43Lakini kwenu isiwe hivyo, ila anayetaka kuwa mkuu kati yenu, sharti awe mtumishi wenu. 44Anayetaka kuwa wa kwanza, sharti awe mtumishi wa wote. 45Maana Mwana wa Mtu hakuja kutumikiwa, ila alikuja kutumikia, na kutoa maisha yake kuwa fidia ya watu wengi."

46Basi, wakafika Yeriko, naye Yesu alipokuwa anatoka katika mji huo akiwa na wanafunzi wake pamoja na umati mkubwa wa watu, kipofu mwombaji aitwaye Bartimayo mwana wa Timayo alikuwa ameketi kando ya barabara. 47Aliposikia kwamba ni Yesu wa Nazareti aliyekuwa anapita mahali hapo, alianza kupaaza sauti, "Yesu, Mwana wa Daudi, nihurumie!" 48Watu wengi walimkemea ili anyamaze, lakini yeye akazidi kupaaza sauti, "Mwana wa Daudi, nihurumie!" 49Yesu alisimama, akasema, "Mwiteni." Basi, wakamwita huyo kipofu, wakamwambia, "Jipe moyo! Simama, anakuita." 50Naye akatupilia mbali vazi lake, akaruka juu, akamwendea Yesu. 51Yesu akamwuliza, "Unataka nikufanyie nini?" Huyo kipofu akamwambia, "Mwalimu, naomba nipate kuona." 52Yesu akamwambia, "Nenda, imani yako imekuponya." Mara huyo kipofu akaweza kuona, akamfuata Yesu njiani.Public Domain Swahili New Testament -- PLEASE MAKE COPIES FOR YOUR FRIENDS, NO ROYALTY DUE.

Bible Hub

Mark 9
Top of Page
Top of Page