Marko 15
Swahili NT
1Kulipopambazuka, makuhani wakuu walifanya shauri pamoja na wazee, walimu wa Sheria na Baraza lote, wakamfunga Yesu pingu, wakampeleka na kumkabidhi kwa Pilato. 2Pilato akamwuliza Yesu, "Je, wewe ni mfalme wa Wayahudi?" Yesu akajibu, "Wewe umesema." 3Makuhani wakuu wakamshtaki Yesu mambo mengi. 4Pilato akamwuliza tena Yesu, "Je, hujibu neno? Tazama wanavyotoa mashtaka mengi juu yako." 5Lakini Yesu hakujibu neno, hata pilato akashangaa.

6Kila wakati wa sikukuu ya Pasaka, Pilato alikuwa na desturi ya kuwafungulia mfungwa mmoja waliyemtaka. 7Basi, kulikuwa na mtu mmoja aitwaye Baraba, ambaye alikuwa amefungwa pamoja na waasi wengine kwa kusababisha uasi na mauaji. 8Watu wengi wakamwendea Pilato wakamwomba awafanyie kama kawaida yake. 9Pilato akawauliza, "Je, mwataka niwafungulieni Mfalme wa Wayahudi?" 10Alisema hivyo kwa sababu alijua wazi kwamba makuhani wakuu walimkabidhi Yesu kwake kwa sababu ya wivu. 11Lakini makuhani wakuu wakawachochea watu wamwombe Pilato awafungulie Baraba. 12Pilato akawauliza tena, "Basi, sasa mwataka nifanye nini na mtu huyu mnayemwita Mfalme wa Wayahudi?" 13Watu wote wakapaaza sauti tena: "Msulubishe!" 14Lakini Pilato akawauliza, "Kwa nini! Amefanya kosa gani?" Lakini wao wakazidi kupaaza sauti, "Msulubishe!" 15Pilato alitaka kuuridhisha huo umati wa watu; basi, akamwachilia Baraba kutoka gerezani. Akaamuru Yesu apigwe viboko, kisha akamtoa asulubiwe.

16Kisha askari walimpeleka Yesu ndani ukumbini, katika ikulu, wakakusanya kikosi kizima cha askari. 17Wakamvika vazi la rangi ya zambarau, wakasokota taji ya miiba, wakamwekea kichwani. 18Wakaanza kumsalimu, "Shikamoo Mfalme wa Wayahudi!" 19Wakampiga kichwani kwa mwanzi, wakamtemea mate; wakampigia magoti na kumsujudia. 20Baada ya kumdhihaki, walimvua lile joho, wakamvika nguo zake, kisha wakampeleka kumsulubisha.

21Walipokuwa njiani, walikutana na mtu mmoja aitwaye Simoni, mwenyeji wa Kurene. Yeye alikuwa baba wa Aleksanda na Rufo, na wakati huo alikuwa akitoka shambani. Basi, wakamlazimisha auchukue msalaba wa Yesu.

22Kisha wakampeleka Yesu mpaka mahali palipoitwa Golgotha, maana yake, "Mahali pa Fuvu la Kichwa." 23Wakampa divai iliyochanganywa na manemane, lakini yeye akaikataa. 24Basi, wakamsulubisha, wakagawana mavazi yake kwa kuyapigia kura waamue nani angepata nini. 25Ilikuwa saa tatu asubuhi walipomsulubisha. 26Na mshtaka wake ulikuwa umeandikwa: "Mfalme wa Wayahudi."

27Pamoja naye waliwasulubisha wanyang'anyi wawili, mmoja upande wake wa kulia na mwingine upande wake wa kushoto. 28Hapo yakatimia Maandiko Matakatifu yanayosema, "Aliwekwa kundi moja na waovu." 29Watu waliokuwa wanapita mahali hapo walimtukana, wakitikisa vichwa vyao na kusema, "Aha! Wewe mwenye kuvunja Hekalu na kulijenga kwa siku tatu! 30Sasa, shuka msalabani ujiokoe mwenyewe!" 31Nao makuhani wakuu pamoja na walimu wa Sheria walimdhihaki wakisema, "Aliwaokoa wengine, lakini kujiokoa mwenyewe hawezi! 32Eti yeye ni Kristo, Mfalme wa Israeli! Basi, na ashuke msalabani ili tuone na kuamini." Hata watu wale waliosulubiwa pamoja naye walimtukana.

33Tangu saa sita mchana mpaka saa tisa kulikuwa giza nchini kote. 34Saa tisa alasiri Yesu akalia kwa sauti kubwa, "Eloi, Eloi, lema sabakthani?" Maana yake, "Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?" 35Baadhi ya watu waliosimama pale waliposikia hivyo, walisema, "Sikiliza! Anamwita Eliya!" 36Mtu mmoja akakimbia, akachovya sifongo katika siki, akaiweka juu ya mwanzi, akampa anywe akisema, "Hebu tuone kama Eliya atakuja kumteremsha msalabani!" 37Yesu akapaaza sauti kubwa, akakata roho. 38Basi, pazia la Hekalu likapasuka vipande viwili toka juu mpaka chini. 39Jemadari mmoja aliyekuwa amesimama mbele yake aliona jinsi Yesu alivyolia kwa sauti na kukata roho, akasema, "Kweli mtu huyu alikuwa Mwana wa Mungu!"

40Walikuwako pia wanawake waliotazama kwa mbali, miongoni mwao akiwa Maria toka mji wa Magdala, Salome, na Maria mama wa kina Yakobo mdogo na Yose. 41Hawa walimfuata Yesu alipokuwa Galilaya na kumtumikia. Kulikuwa na wanawake wengine wengi waliokuja Yerusalemu pamoja naye.

42Wakati wa jioni ulikuwa umekwisha fika. Hiyo ilikuwa siku ya Maandalio, yaani siku inayotangulia Sabato. 43Hapo akaja Yosefu mwenyeji wa Armathaya, mjumbe wa Baraza Kuu, aliyeheshimika sana. Yeye pia alikuwa anatazamia kuja kwa Ufalme wa Mungu. Basi, alimwendea Pilato bila uoga, akaomba apewe mwili wa Yesu. 44Pilato alishangaa kusikia kwamba Yesu alikuwa amekwisha kufa. Basi, akamwita jemadari, akamwuliza kama Yesu alikuwa amekufa kitambo. 45Pilato alipoarifiwa na huyo jemadari kwamba Yesu alikuwa amekwisha kufa, akamruhusu Yosefu auchukue mwili wake. 46Hapo Yosefu akanunua sanda ya kitani, akauteremsha chini huo mwili, akauzungushia sanda. Akauweka katika kaburi lililokuwa limechongwa mwambani, kisha akavingirisha jiwe kubwa mbele ya mlango. 47Nao Maria Magdalene na Maria mama yake Yose walipaona hapo alipolazwa.



Public Domain Swahili New Testament -- PLEASE MAKE COPIES FOR YOUR FRIENDS, NO ROYALTY DUE.

Bible Hub

Mark 14
Top of Page
Top of Page