Swahili NT 1Yesu alianza kusema nao kwa mifano: "Mtu mmoja alilima shamba la mizabibu. Akalizungushia ukuta, na katikati yake akachimba kisima cha kusindikia divai, akajenga mnara pia. Akalikodisha shamba hilo kwa wakulima, akasafiri hadi nchi ya mbali.
2Wakati wa mavuno, alimtuma mtumishi wake kwa wale wakulima akamletee sehemu ya mazao ya shamba lake.
3Wale wakulima wakamkamata, wakampiga, wakamrudisha mikono mitupu.
4Akatuma tena mtumishi mwingine; huyu wakamuumiza kichwa na kumtendea vibaya.
5Mwenye shamba akatuma mtumishi mwingine tena, na huyo wakamuua. Wengine wengi waliotumwa, baadhi yao walipigwa, na wengi wakauawa.
6Alibakiwa bado na mtu mmoja, yaani mwanawe mpendwa. Mwishowe akamtuma huyo akisema, Watamheshimu mwanangu.
7Lakini hao wakulima wakaambiana, Huyu ndiye mrithi, basi, tumuue ili urithi wake uwe wetu!
8Kwa hiyo wakamkamata, wakamuua na kumtupa nje ya lile shamba la mizabibu.
9Basi, mwenye shamba atafanya nini? Atakuja kuwaangamiza hao wakulima na kulikodisha hilo shamba la mizabibu kwa watu wengine. 10Je, hamjasoma Maandiko haya? Jiwe walilokataa waashi sasa limekuwa jiwe kuu la msingi. 11Bwana ndiye aliyefanya jambo hili, nalo ni la ajabu sana kwetu." 12Makuhani wakuu, walimu wa Sheria na wazee walifahamu ya kwamba mfano huo ulikuwa unawahusu. Kwa hiyo walijaribu kumtia nguvuni, lakini waliogopa umati wa watu. Basi, wakamwacha wakaenda zao. 13Basi, baadhi ya Mafarisayo na wafuasi wa kikundi cha Herode walitumwa ili wamtege Yesu kwa maneno yake. 14Wakamwendea, wakamwambia, "Mwalimu, tunajua kwamba wewe ni mtu mwaminifu unayesema ukweli mtupu, wala humjali mtu yeyote. Wala cheo cha mtu si kitu kwako, lakini wafundisha ukweli kuhusu njia ya Mungu. Je, ni halali kulipa kodi kwa Kaisari, au la? Tulipe au tusilipe?" 15Lakini Yesu alijua unafiki wao, akawaambia, "Mbona mnanijaribu? Nionyesheni sarafu." 16Wakamwonyesha. Naye akawauliza, "Sura na chapa hii ni ya nani?" Wakamjibu, "Ni ya Kaisari." 17Basi, Yesu akawaambia, "Mpeni Kaisari yaliyo yake Kaisari na Mungu yaliyo yake Mungu." Wakashangazwa sana naye. 18Masadukayo wasemao kwamba hakuna ufufuo walimwendea Yesu, wakamwuliza, 19Mwalimu, Mose alituagiza hivi: Mtu akifa na kuacha mke bila mtoto, ndugu yake lazima amchukue huyo mama mjane amzalie watoto ndugu yake marehemu. 20Basi, kulikuwa na ndugu saba. Wa kwanza alioa, akafa bila kuacha mtoto. 21Ndugu wa pili akamwoa huyo mjane, naye pia akafa bila kuacha mtoto; na ndugu watatu hali kadhalika. 22Wote saba walikufa bila kuacha mtoto. Mwishowe yule mama mjane naye akafa. 23Basi, siku watu watakapofufuka, mama huyo atakuwa mke wa nani? Maana wote saba walikuwa wamemwoa." 24Yesu akawaambia, "Ninyi mmekosea sana, kwa sababu hamjui Maandiko Matakatifu wala nguvu ya Mungu. 25Maana wafu watakapofufuka, hawataoa wala kuolewa; watakuwa kama malaika wa mbinguni. 26Lakini kuhusu kufufuliwa kwa wafu, je, hamjasoma kitabu cha Mose katika sehemu inayohusu kile kichaka kilichokuwa kinawaka moto? Mungu alimwambia Mose, Mimi ni Mungu wa Abrahamu, Mungu wa Isaka, na Mungu wa Yakobo. 27Basi, yeye si Mungu wa wafu, bali ni Mungu wa walio hai. Ninyi mmekosea sana!" 28Mmojawapo wa walimu wa Sheria alifika, akasikia mabishano yao. Alipoona kwamba Yesu aliwajibu vyema, akajitokeza akamwuliza, "Katika amri zote ni ipi iliyo ya kwanza?" 29Yesu akamjibu, "Ya kwanza ndiyo hii: Sikiliza, Israeli! Bwana Mungu wetu ndiye peke yake Bwana. 30Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, kwa roho yako yote, kwa akili yako yote na kwa nguvu zako zote. 31Na ya pili ndiyo hii: Mpende jirani yako kama unavyojipenda mwenyewe. Hakuna amri nyingine iliyo kuu kuliko hizi." 32Basi, yule mwalimu wa Sheria akamwambia, "Vyema Mwalimu! Umesema kweli kwamba Mungu ni mmoja tu wala hakuna mwingine ila yeye. 33Na ni lazima mtu kumpenda Mungu kwa moyo wote, kwa akili yote, na kwa nguvu zote, na kumpenda jirani yake kama anavyojipenda mwenyewe. Jambo hili ni muhimu zaidi kuliko dhabihu na sadaka zote za kuteketezwa." 34Yesu alipoona kwamba huyu mtu alimjibu kwa ujasiri, akamwambia, "Wewe huko mbali na Ufalme wa Mungu." Baada ya hayo, hakuna mtu aliyethubutu tena kumwuliza kitu. 35Wakati Yesu alipokuwa akifundisha Hekaluni, aliuliza, "Mbona walimu wa Sheria wanasema ya kwamba Kristo ni mwana wa Daudi? 36Daudi mwenyewe akiongozwa na Roho Mtakatifu alisema: Bwana alimwambia Bwana wangu: Keti upande wangu wa kulia, Mpaka nitakapowaweka adui zako chini ya miguu yako." 37Daudi mwenyewe anamwita Kristo Bwana. Basi, Kristo atakuwaje mwanae? Umati wa watu ulikuwa ukimsikiliza kwa furaha. 38Katika mafundisho yake, Yesu alisema, "Jihadharini na walimu wa Sheria ambao hupenda kupitapita wamejivalia kanzu ndefu na kusalimiwa na watu kwa heshima sokoni; hupenda kuketi mahali pa heshima katika masunagogi, 39na kuchukua nafasi za heshima katika karamu. 40Huwanyonya wajane huku wakijisingizia kusali sala ndefu. Siku ya hukumu watapata adhabu kali!" 41Yesu alikuwa ameketi karibu na sanduku la hazina. Akawa anatazama jinsi watu wengi walivyokuwa wakitoa fedha na kuzitia katika hazina ya Hekalu. Matajiri wengi walitoa fedha nyingi. 42Hapo akaja mama mmoja mjane maskini, akatoa sarafu mbili ndogo za fedha. 43Yesu akawaita wanafunzi wake, akawaambia, "Kweli nawaambieni, huyu mama mjane maskini ametoa zaidi kuliko wengine wote waliotia fedha katika sanduku la hazina. 44Maana wote walitoa kutokana na ziada ya mali zao, lakini huyu mama, ingawa ni maskini, ametoa yote aliyokuwa nayo, ametoa kila kitu alichohitaji kwa kuishi." Public Domain Swahili New Testament -- PLEASE MAKE COPIES FOR YOUR FRIENDS, NO ROYALTY DUE. Bible Hub |