Luka 4
Swahili NT
1Yesu alitoka katika mto Yordani akiwa amejaa Roho Mtakatifu, akaongozwa na Roho mpaka jangwani. 2Huko alijaribiwa na Ibilisi kwa muda wa siku arubaini. Wakati huo wote hakula chochote, na baada ya siku hizo akasikia njaa. 3Ndipo Ibilisi akamwambia, "Kama wewe ni Mwana wa Mungu, amuru jiwe hili liwe mkate." 4Yesu akamjibu, "Imeandikwa: Mtu haishi kwa mkate tu."

5Kisha Ibilisi akamchukua hadi mahali pa juu, akamwonyesha kwa mara moja falme zote za ulimwengu. Huyo Shetani akamwambia, 6Nitakupa uwezo juu ya falme zote hizi na fahari zake, kwa maana nimepewa hivi vyote; nikitaka kumpa mtu ninaweza. 7Hivi vyote vitakuwa mali yako wewe, kama ukiniabudu." 8Yesu akamjibu, "Imeandikwa: Utamwabudu Bwana Mungu wako, na utamtumikia yeye peke yake."

9Ibilisi akamchukua mpaka Yerusalemu, kwenye mnara wa Hekalu, akamwambia, "Kama wewe ni Mwana wa Mungu,

10kwa maana imeandikwa: Atawaamuru malaika wake wakulinde,

11na tena, Watakuchukua mikononi mwao usije ukajikwaa mguu wako kwenye jiwe."

12Lakini Yesu akamjibu, "Imeandikwa: Usimjaribu Bwana Mungu wako."

13Ibilisi alipokwishamjaribu kwa kila njia, akamwacha kwa muda.

14Yesu alirudi Galilaya akiwa amejaa nguvu za Roho Mtakatifu, na habari zake zikaenea katika sehemu zote za jirani. 15Naye akawa anawafundisha watu katika masunagogi yao, akasifiwa na wote.

16Basi, Yesu alikwenda Nazareti, mahali alipolelewa, na siku ya Sabato, aliingia katika sunagogi, kama ilivyokuwa desturi yake. Akasimama ili asome Maandiko Matakatifu kwa sauti. 17Akapokea kitabu cha nabii Isaya, akakifungua na akakuta mahali palipoandikwa:

18Roho wa Bwana yu juu yangu, kwani amenipaka mafuta niwahubirie maskini Habari Njema. Amenituma niwatangazie mateka watapata uhuru, vipofu watapata kuona tena; amenituma niwakomboe wanaoonewa,

19na kutangaza mwaka wa neema ya Bwana." 20Baada ya kusoma, akafunga kile kitabu, akampa mtumishi, kisha akaketi; watu wote wakamkodolea macho. 21Naye akaanza kuwaambia, "Andiko hili mlilosikia likisomwa, limetimia leo." 22Wote wakavutiwa sana naye, wakastaajabia maneno mazuri aliyosema. Wakanena, "Je, huyu si mwana wa Yosefu?" 23Naye akawaambia, "Bila shaka mtaniambia msemo huu: Mganga jiponye mwenyewe, na pia mtasema: Yote tuliyosikia umeyafanya kule Kafarnaumu, yafanye hapa pia katika kijiji chako." 24Akaendelea kusema, "Hakika nawaambieni, nabii hatambuliwi katika kijiji chake. 25Lakini, sikilizeni! Kweli kulikuwa na wajane wengi katika nchi ya Israeli nyakati za Eliya. Wakati huo mvua iliacha kunyesha kwa muda wa miaka mitatu na nusu; kukawa na njaa kubwa katika nchi yote. 26Hata hivyo, Eliya hakutumwa kwa mjane yeyote ila kwa mwanamke mjane wa Sarepta, Sidoni. 27Tena, katika nchi ya Israeli nyakati za Elisha kulikuwa na wenye ukoma wengi. Hata hivyo, hakuna yeyote aliyetakaswa ila tu Naamani, mwenyeji wa Siria." 28Wote waliokuwa katika lile sunagogi waliposikia hayo walikasirika sana. 29Wakasimama, wakamtoa nje ya mji wao uliokuwa umejengwa juu ya kilima, wakampeleka mpaka kwenye ukingo wa kilima hicho ili wamtupe chini. 30Lakini Yesu akapita katikati yao, akaenda zake.

31Kisha Yesu akashuka mpaka Kafarnaumu katika mkoa wa Galilaya, akawa anawafundisha watu siku ya Sabato. 32Wakastaajabia uwezo aliokuwa nao katika kufundisha. 33Na katika lile sunagogi kulikuwa na mtu aliyekuwa amepagawa na roho ya pepo mchafu; akapiga ukelele wa kuziba masikio: 34We! Yesu wa Nazareti! Kwa nini unatuingilia? Je, umekuja kutuangamiza? Ninakufahamu wewe ni nani. Wewe ni mjumbe Mtakatifu wa Mungu! 35Lakini Yesu akamkemea huyo pepo akisema: "Nyamaza! Mtoke mtu huyu!" Basi, huyo pepo baada ya kumwangusha yule mtu chini, akamtoka bila kumdhuru hata kidogo. 36Watu wote wakashangaa, wakawa wanaambiana, "Hili ni jambo la ajabu, maana kwa uwezo na nguvu anawaamuru pepo wachafu watoke, nao wanatoka!" 37Habari zake zikaenea mahali pote katika mkoa ule.

38Yesu alitoka katika lile sunagogi, akaenda nyumbani kwa Simoni. Mama mmoja, mkwewe Simoni, alikuwa na homa kali; wakamwomba amponye. 39Yesu akaenda akasimama karibu naye, akaikemea ile homa, nayo ikamwacha. Mara yule mama akainuka, akawatumikia.

40Jua lilipokuwa linatua, wote waliokuwa na wagonjwa wao mbalimbali waliwaleta kwake; naye akaweka mikono yake juu ya kila mmoja wao, akawaponya wote. 41Pepo waliwatoka watu wengi, wakapiga kelele wakisema: "Wewe u Mwana wa Mungu!" Lakini Yesu akawakemea, wala hakuwaruhusu kusema, maana walimfahamu kwamba yeye ndiye Kristo.

42Kesho yake asubuhi Yesu aliondoka akaenda mahali pa faragha. Watu wakawa wanamtafuta, na walipofika mahali alipokuwa, wakajaribu kumzuia ili asiondoke kwao. 43Lakini yeye akawaambia, "Ninapaswa kuhubiri Habari Njema za Ufalme wa Mungu katika miji mingine pia, maana nilitumwa kwa ajili hiyo."

44Akawa anahubiri katika masunagogi ya Yudea.Public Domain Swahili New Testament -- PLEASE MAKE COPIES FOR YOUR FRIENDS, NO ROYALTY DUE.

Bible Hub

Luke 3
Top of Page
Top of Page