Ufunua was Yohana 2
Swahili NT
1Kwa malaika wa kanisa la Efeso andika hivi: Huu ndio ujumbe kutoka kwake yeye ashikaye nyota saba katika mkono wake wa kulia, na ambaye hutembea katikati ya vinara saba vya taa vya dhahabu.

2Najua mambo yako yote; najua bidii yako na uvumilivu wako. Najua kwamba huwezi kuwavumilia watu waovu, na kwamba umewapima wale wanaojisemea kuwa mitume na kumbe sio, ukagundua kwamba ni waongo. 3Wewe unayo saburi, umestahimili taabu nyingi kwa ajili ya jina langu, wala hukuvunjika moyo. 4Lakini ninayo hoja moja juu yako: wewe hunipendi tena sasa kama pale awali. 5Basi, pakumbuke pale ulipokuwa kabla ya kuanguka, ukayaache madhambi yako, na kufanya kama ulivyofanya pale awali. La sivyo, naja kwako na kukiondoa kinara chako mahali pake. 6Lakini nakusifu juu ya kitu kimoja: wewe unayachukia wanayoyatenda Wanikolai kama ninavyoyachukia mimi. 7Aliye na masikio, basi, na asikie yale Roho anayoyaambia makanisa! Wale wanaoshinda nitawapa haki ya kula matunda ya mti wa uzima ulioko ndani ya bustani ya Mungu.

8Kwa malaika wa kanisa la Smurna andika hivi: Huu ndio ujumbe kutoka kwake yeye wa kwanza na wa mwisho, ambaye alikufa na akaishi tena.

9Najua taabu zako; najua pia umaskini wako, ingawaje kwa kweli wewe ni tajiri; najua kashfa walizokufanyia wale wanaojiita Wayahudi lakini si Wayahudi wa kweli, bali ni kundi lake Shetani. 10Usiogope hata kidogo yale ambayo itakulazimu kuteseka. Sikiliza! Ibilisi anataka kuwajaribu kwa kuwatia baadhi yenu gerezani; nanyi mtapata dhiki kwa muda wa siku kumi. Muwe waaminifu hata mpaka kufa, nami nitawapeni taji ya uzima. 11Aliye na masikio, basi, na asikie yale Roho anayoyaambia makanisa! Wale wanaoshinda hawataumizwa na kifo cha pili.

12Kwa malaika wa kanisa la Pergamoni andika hivi: Huu ndio ujumbe wake yeye aliye na upanga mkali wenye kuwili.

13Najua unakoishi: Wewe unaishi kwenye makao makuu ya Shetani! Lakini bado unashikilia jina langu; hukuikana imani yako kwangu hata siku zile Antipa shahidi wangu mwaminifu, alipouawa pale mahali anapoishi Shetani. 14Lakini ninayo machache dhidi yako: baadhi yenu ni wafuasi wa Balaamu aliyemfundisha Balaki kuwatega wana wa Israeli wale vyakula vilivyotambikiwa sanamu za kufanya uzinzi. 15Vivyo hivyo, wako pia miongoni mwenu watu wanaofuata mafundisho ya Wanikolai. 16Basi, achana na madhambi yako. La sivyo, nitakuja kwako upesi na kupigana na watu hao kwa upanga utokao kinywani mwangu. 17Aliye na masikio, basi, na asikie yale Roho anayoyaambia makanisa! Wale wanaoshinda nitawapa ile mana iliyofichika. Nitawapa pia jiwe jeupe lililoandikwa jina jipya ambalo hakuna mtu aliyelijua isipokuwa tu wale wanaolipokea.

18Kwa malaika wa kanisa la Thuatira andika hivi: Huu ndio ujumbe wa Mwana wa Mungu, ambaye macho yake yametameta kama moto, na miguu yake inang'aa kama shaba iliyosuguliwa.

19Najua mambo yako yote. Najua upendo wako, imani yako, utumishi wako na uvumilivu wako. Wewe unafanya vizuri zaidi sasa kuliko pale awali. 20Lakini nina hoja moja juu yako: wewe unamvumilia yule mwanamke Yezabeli anayejiita nabii wa Mungu. Yeye huwafundisha na kuwapotosha watumishi wangu wafanye uzinzi na kula vyakula vilivyotambikiwa sanamu. 21Nimempa muda wa kutubu dhambi zake, lakini hataki kuachana na uzinzi wake. 22Sikiliza! Sasa namtupa kitandani ambapo yeye pamoja na wote waliofanya uzinzi naye watapatwa na mateso makali. Naam, nitafanya hivyo, kama wasipotubu matendo yao mabaya waliyotenda naye. 23Tena nitawaua wafuasi wake, ili makanisa yote yatambue kwamba mimi ndiye ninayechunguza mioyo na fikira za watu. 24Lakini ninyi wengine mlioko huko Thuatira ambao hamfuati mafundisho yake Yezabeli, na ambao hamkujifunza kile wanachokiita Siri ya Shetani, nawaambieni kwamba sitawapeni mzigo mwingine. 25Lazima mzingatie yale mliyo nayo sasa mpaka nitakapokuja. 26Wanaoshinda, na wale watakaozingatia mpaka mwisho kutenda ninayotaka, nitawapa mamlaka juu ya mataifa. 27Naam, nitawapa uwezo uleule nilioupokea kwa Baba: yaani, watayatawala mataifa kwa fimbo ya chuma na kuyavunjavunja kama chombo cha udongo. 28Tena nitawapa nyota ya asubuhi. 29Aliye na masikio, basi, na ayasikie yale Roho anayoyaambia makanisa!Public Domain Swahili New Testament -- PLEASE MAKE COPIES FOR YOUR FRIENDS, NO ROYALTY DUE.

Bible Hub

Revelation 1
Top of Page
Top of Page