Luka 1
Swahili NT
1Mheshimiwa Theofilo: Watu wengi wamejitahidi kuandika juu ya mambo yale yaliyotendeka kati yetu. 2Waliandika kama tulivyoelezwa na wale walioyaona kwa macho yao tangu mwanzo, na waliotangaza ujumbe huo. 3Inafaa nami pia, Mheshimiwa, baada ya kuchunguza kwa makini mambo yote tangu mwanzo, nikuandikie kwa mpango, 4ili nawe uweze kujionea mwenyewe ukweli wa mambo yale uliyofundishwa.

5Wakati Herode alipokuwa mfalme wa Yudea, kulikuwa na kuhani mmoja jina lake Zakaria, wa kikundi cha Abia. Mke wake alikuwa anaitwa Elisabeti, naye alikuwa wa ukoo wa kuhani Aroni. 6Wote wawili walikuwa wanyofu mbele ya Mungu, wakiishi kwa kufuata amri na maagizo yote ya Bwana bila lawama. 7Lakini hawakuwa wamejaliwa watoto kwa vile Elisabeti alikuwa tasa, nao wote wawili walikuwa wazee sana.

8Siku moja, ilipokuwa zamu yake ya kutoa huduma ya ukuhani mbele ya Mungu, 9Zakariya alichaguliwa kwa kura, kama ilivyokuwa desturi, kuingia hekaluni ili afukize ubani. 10Watu, umati mkubwa, walikuwa wamekusanyika nje wanasali wakati huo wa kufukiza ubani. 11Malaika wa Bwana akamtokea humo ndani, akasimama upande wa kulia wa madhabahu ya kufukizia ubani. 12Zakariya alipomwona alifadhaika, hofu ikamwingia. 13Lakini malaika akamwambia, "Zakariya, usiogope, kwa maana sala yako imesikilizwa, na Elisabeti mkeo atakuzalia mtoto wa kiume, nawe utampa jina Yohane. 14Utakuwa na furaha kubwa na watu wengi watashangilia kwa sababu ya kuzaliwa kwake. 15Atakuwa mkuu mbele ya Bwana. Hatakunywa divai wala kileo, atajazwa Roho Mtakatifu tangu tumboni mwa mama yake. 16Atawaelekeza wengi wa watu wa Israeli kwa Bwana Mungu wao. 17Atamtangulia Bwana akiongozwa na nguvu na roho kama Eliya. Atawapatanisha kina baba na watoto wao; atawafanya wasiotii wawe na fikira za uadilifu, na hivyo amtayarishie Bwana watu wake."

18Zakariya akamwambia huyo malaika, "Ni kitu gani kitakachonihakikishia jambo hilo? Mimi ni mzee, hali kadhalika na mke wangu." 19Malaika akamjibu, "Mimi ni Gabrieli, nisimamaye mbele ya Mungu, na nimetumwa niseme nawe, nikuletee hii habari njema. 20Sikiliza, utakuwa bubu kwa sababu huyasadiki haya maneno yatakayotimia kwa wakati wake. Hutaweza kusema mpaka hayo niliyokuambia yatakapotimia."

21Wakati huo, wale watu walikuwa wanamngoja Zakariya huku wakishangaa juu ya kukawia kwake Hekaluni. 22Alipotoka nje, hakuweza kusema nao. Ikawa dhahiri kwao kwamba alikuwa ameona maono Hekaluni. Lakini akawa anawapa ishara kwa mikono, akabaki bubu. 23Zamu yake ya kuhudumu ilipokwisha, alirudi nyumbani.

24Baadaye Elisabeti mkewe akapata mimba. Akajificha nyumbani kwa muda wa miezi mitano, akisema: 25Hivi ndivyo alivyonitendea Bwana; ameniangalia na kuniondolea aibu niliyokuwa nayo mbele ya watu.

26Mnamo mwezi wa sita, malaika Gabrieli alitumwa na Mungu aende kwenye mji uitwao Nazareti huko Galilaya, 27kwa msichana mmoja aitwaye Maria, mchumba wa mtu mmoja jina lake Yosefu, wa ukoo wa Daudi. 28Malaika akamwendea, akamwambia, "Salamu Maria! Umejaliwa neema nyingi! Bwana yu pamoja nawe." 29Maria aliposikia maneno hayo alifadhaika sana, akawaza: maneno haya yanamaanisha nini? 30Malaika akamwambia, "Usiogope Maria, kwa maana Mungu amekujalia neema. 31Utachukua mimba, utamzaa mtoto wa kiume na utampa jina Yesu. 32Yeye atakuwa mkuu na ataitwa Mwana wa Mungu Mkuu. Bwana Mungu atampa kiti cha mfalme Daudi, babu yake. 33Kwa hivyo atautawala ukoo wa Yakobo milele, na ufalme wake hautakuwa na mwisho." 34Maria akamjibu, "Yatawezekanaje hayo, hali mimi ni bikira?" 35Malaika akamjibu, "Roho Mtakatifu atakushukia, na uwezo wake Mungu Mkuu utakujia kama kivuli; kwa sababu hiyo, mtoto atakayezaliwa ataitwa Mtakatifu, Mwana wa Mungu. 36Ujue pia kwamba hata Elisabeti, jamaa yako, naye amepata mimba ingawa ni mzee, na sasa ni mwezi wa sita kwake yeye ambaye watu walimfahamu kuwa tasa. 37Kwa maana hakuna jambo lisilowezekana kwa Mungu." 38Maria akasema, "Mimi ni mtumishi wa Bwana, nitendewe kama ulivyosema." Kisha yule malaika akaenda zake.

39Siku kadhaa baadaye, Maria alifunga safari akaenda kwa haraka hadi mji mmoja ulioko katika milima ya Yuda. 40Huko, aliingia katika nyumba ya Zakariya, akamsalimu Elisabeti. 41Mara tu Elisabeti aliposikia sauti ya Maria, mtoto mchanga tumboni mwake Elisabeti akaruka. Naye Elisabeti akajazwa Roho Mtakatifiu, 42akasema kwa sauti kubwa, "Umebarikiwa kuliko wanawake wote, naye utakayemzaa amebarikiwa. 43Mimi ni nani hata mama wa Bwana wangu afike kwangu? 44Nakwambia, mara tu niliposikia sauti yako, mtoto mchanga tumboni mwangu aliruka kwa furaha. 45Heri yako wewe uliyesadiki kwamba yatatimia yale Bwana aliyokwambia."

46Naye Maria akasema,

47Moyo wangu wamtukuza Bwana, roho yangu inafurahi kwa sababu ya Mungu Mwokozi wangu.

48Kwa kuwa amemwangalia kwa huruma mtumishi wake mnyenyekevu. Hivyo tangu sasa watu wote wataniita mwenye heri.

49Kwa kuwa Mwenyezi Mungu amenitendea makuu, jina lake ni takatifu.

50Huruma yake kwa watu wanaomcha hudumu kizazi hata kizazi.

51Amefanya mambo makuu kwa mkono wake: amewatawanya wenye kiburi katika mawazo ya mioyo yao;

52amewashusha wenye nguvu kutoka vitu vyao vya enzi, akawakweza wanyenyekevu.

53Wenye njaa amewashibisha mema, matajiri amewaacha waende mikono mitupu.

54Amemsaidia Israeli mtumishi wake, akikumbuka huruma yake.

55Kama alivyowaahidia wazee wetu Abrahamu na wazawa wake hata milele."

56Maria alikaa na Elisabeti kwa muda upatao miezi mitatu, halafu akarudi nyumbani kwake.

57Wakati wa kujifungua kwake Elisabeti ulifika, akajifungua mtoto wa kiume. 58Jirani na watu wa jamaa yake walipopata habari kwamba Bwana amemwonea huruma kubwa, walifurahi pamoja naye.

59Halafu siku ya nane walifika kumtahiri mtoto, wakataka kumpa jina la baba yake, Zakariya. 60Lakini mama yake akasema, "La, sivyo, bali ataitwa Yohane." 61Wakamwambia, "Mbona hakuna yeyote katika ukoo wake mwenye jina hilo?" 62Basi, wakamwashiria baba yake wapate kujua alitaka mtoto wake apewe jina gani. 63Naye akaomba kibao cha kuandikia, akaandika hivi: "Yohane ndilo jina lake." Wote wakastaajabu. 64Papo hapo midomo na ulimi wake Zakariya vikafunguliwa, akawa anaongea akimsifu Mungu. 65Hofu ikawaingia jirani wote, na habari hizo zikaenea kila mahali katika milima ya Yudea. 66Wote waliosikia mambo hayo waliyatafakari mioyoni mwao wakisema: "Mtoto huyu atakuwa mtu wa namna gani?" Maana, hakika nguvu ya Bwana ilikuwa pamoja naye.

67Zakariya, baba yake mtoto, akajazwa Roho Mtakatifu, akatamka ujumbe wa Mungu:

68Asifiwe Bwana Mungu wa Israeli, kwani amekuja kuwasaidia na kuwakomboa watu wake.

69Ametupatia Mwokozi shujaa, mzawa wa Daudi mtumishi wake.

70Aliahidi hapo kale kwa njia ya manabii wake watakatifu,

71kwamba atatuokoa mikononi mwa adui zetu na kutoka mikononi mwa wote wanaotuchukia.

72Alisema atawahurumia wazee wetu, na kukumbuka agano lake takatifu.

73Kiapo alichomwapia Abrahamu baba yetu, ni kwamba atatujalia sisi

74tukombolewe kutoka adui zetu, tupate kumtumikia bila hofu,

75kwa unyofu na uadilifu mbele yake, siku zote za maisha yetu.

76Nawe mwanangu, utaitwa, nabii wa Mungu Mkuu, utamtangulia Bwana kumtayarishia njia yake;

77kuwatangazia watu kwamba wataokolewa kwa kuondolewa dhambi zao.

78Mungu wetu ni mpole na mwenye huruma. Atasababisha pambazuko angavu la ukombozi litujie kutoka juu,

79na kuwaangazia wote wanaokaa katika giza kuu la kifo, aongoze hatua zetu katika njia ya amani."

80Mtoto akakua, akapata nguvu rohoni. Alikaa jangwani mpaka alipojionyesha rasmi kwa watu wa Israeli.Public Domain Swahili New Testament -- PLEASE MAKE COPIES FOR YOUR FRIENDS, NO ROYALTY DUE.

Bible Hub

Mark 16
Top of Page
Top of Page