1 Wathesalonike 4
Swahili NT
1Hatimaye, ndugu zangu, mmejifunza kutoka kwetu namna mnavyopaswa kuishi ili kumpendeza Mungu. Na kweli mmekuwa mnaishi hivyo. Sasa tunawaombeni na kuwasihi kwa jina la Bwana Yesu mfanye vema zaidi. 2Maana mnayajua yale maagizo tuliyowapeni kwa mamlaka ya Bwana Yesu. 3Mungu anataka ninyi muwe watakatifu na mjiepushe kabisa na maisha ya zinaa. 4Kila mwanamume anapaswa kujua namna ya kuishi na mkewe kwa utakatifu na heshima, 5na si kwa tamaa mbaya kama watu wa mataifa mengine wasiomjua Mungu. 6Basi, mtu yeyote asimkosee au kumpunja mwenzake kuhusu jambo hili. Tulikwisha waambieni hayo na kuwaonya kwamba Bwana atawaadhibu wanaofanya mambo hayo. 7Mungu hakutuita tuishi maisha ya zinaa, bali tuishi katika utakatifu. 8Kwa hiyo basi, anayedharau mafundisho hayo hamdharau mtu, bali amdharau Mungu mwenyewe anayewapeni Roho wake Mtakatifu.

9Hakuna haja ya kuwaandikieni juu ya kuwapenda ndugu zenu waumini. Ninyi wenyewe mmefundishwa na Mungu namna mnavyopaswa kupendana. 10Na mmekuwa mkiwatendea hivyo ndugu zenu wote kila mahali katika Makedonia. Basi, ndugu tunawaombeni mfanye hata zaidi. 11Muwe na nia ya kuishi maisha ya utulivu, kila mmoja ashughulikie mambo yake mwenyewe na afanye kazi kwa mikono yake mwenyewe kama tulivyowaagiza pale awali. 12Kwa namna hiyo mtajipatia sifa nzuri kutoka kwa wale wasio Wakristo, na hamtakuwa na lazima ya kuwategemea wengine kwa mahitaji yenu.

13Ndugu, twataka mjue ukweli kuhusu wale ambao wamekwisha fariki dunia, ili msipatwe na huzuni kama watu wengine wasio na matumaini. 14Sisi tunaamini kwamba Yesu alikufa, akafufuka; na hivyo sisi tunaamini kwamba Mungu atawaleta pamoja na Yesu wale wote waliofariki wakiwa wanamwamini. 15Hili tunalowaambieni ni fundisho la Bwana; sisi tulio hai, ambao tutakuwa tumebaki, wakati Bwana atakapokuja, hakika hatutawatangulia wale waliokwisha fariki dunia. 16Maana patatolewa amri, sauti ya malaika mkuu, sauti ya tarumbeta ya Mungu, naye Bwana mwenyewe atashuka kutoka mbinguni. Ndipo wale waliokufa wakiwa wanamwamini Kristo watafufuliwa kwanza. 17Kisha sisi tulio hai wakati huo tutakusanywa pamoja nao katika mawingu kumlaki Bwana hewani. Na hivyo tutakuwa daima pamoja na Bwana. 18Basi, farijianeni kwa maneno haya.Public Domain Swahili New Testament -- PLEASE MAKE COPIES FOR YOUR FRIENDS, NO ROYALTY DUE.

Bible Hub

1 Thessalonians 3
Top of Page
Top of Page