Matayo 4
Swahili NT
1Kisha Roho alimwongoza Yesu mpaka jangwani ili ajaribiwe na Ibilisi. 2Akafunga siku arubaini mchana na usiku, na mwishowe akaona njaa. 3Basi, mshawishi akamjia, akamwambia, "Ikiwa wewe ni Mwana wa Mungu, amuru mawe haya yawe mikate." 4Yesu akamjibu, "Imeandikwa katika Maandiko Matakatifu: Binadamu hataishi kwa mikate tu, ila kwa kila neno asemalo Mungu."

5Kisha Ibilisi akamchukua mpaka Yerusalemu, mji mtakatifu, akamweka juu ya mnara wa hekalu,

6akamwambia, "Ikiwa wewe ni Mwana wa Mungu, jitupe chini; maana imeandikwa: Mungu atawaamuru malaika wake kwa ajili yako; watakuchukua mikononi mwao, usije ukajikwaa kwenye jiwe."

7Yesu akamwambia, "Imeandikwa pia: Usimjaribu Bwana, Mungu wako."

8Kisha Ibilisi akamchukua mpaka juu ya mlima mrefu, akamwonyesha falme zote za ulimwengu na fahari zake, 9akamwambia, "Hivi vyote nitakupa kama tu ukipiga magoti na kuniabudu." 10Hapo, Yesu akamwambia, "Nenda zako Shetani! Imeandikwa: Utamwabudu Bwana Mungu wako na kumtumikia yeye peke yake." 11Basi, Ibilisi akamwacha, na malaika wakaja, wakamhudumia.

12Yesu aliposikia kwamba Yohane ametiwa gerezani alikwenda Galilaya. 13Aliondoka Nazareti, akaenda Kafarnaumu, mji ulio kando ya bahari ya Genesareti, mpakani mwa wilaya za Zabuloni na Naftali, akakaa huko. 14Ndivyo lilivyotimia lile neno lililosemwa kwa njia ya nabii Isaya:

15Nchi ya Zabuloni na nchi ya Naftali, kuelekea baharini ng'ambo ya mto Yordani, Galilaya nchi ya watu wa Mataifa!

16Watu waliokaa gizani wameona mwanga mkubwa. Nao walioishi katika nchi ya giza na kivuli cha kifo, mwanga umewaangazia!"

17Tangu wakati huo Yesu alianza kuhubiri akisema, "Tubuni, maana ufalme wa mbinguni umekaribia!"

18Yesu alipokuwa anatembea kando ya ziwa Galilaya, aliwaona ndugu wawili wavuvi; Simoni (aitwae Petro) na Andrea, ndugu yake; walikuwa wakivua samaki kwa nyavu ziwani. 19Basi, akawaambia, "Nifuateni, nami nitawafanya ninyi wavuvi wa watu." 20Mara wakaziacha nyavu zao, wakamfuata. 21Alipokwenda mbele kidogo, aliwaona ndugu wengine wawili: Yakobo na Yohane, wana wa Zebedayo. Hao walikuwa ndani ya mashua pamoja na baba yao Zebedayo, wakitengeneza nyavu zao. Basi Yesu akawaita, 22nao mara wakaiacha mashua pamoja na baba yao, wakamfuata.

23Yesu alikuwa anakwenda kila mahali wilayani Galilaya, akifundisha katika masunagogi na kuhubiri Habari Njema juu ya ufalme wa Mungu. Aliponya kila namna ya maradhi na magonjwa waliyokuwa nayo watu.

24Habari zake zikaenea katika mkoa wote wa Siria. Wagonjwa wote wenye maradhi ya kila namna na wale waliosumbuliwa na kila namna ya taabu: waliopagawa na pepo, wenye kifafa na watu waliokuwa wamelemaa, walipelekwa kwake; naye akawaponya wote. 25Makundi mengi ya watu kutoka Galilaya, Dekapoli, Yerusalemu, Yudea na ng'ambo ya mto Yordani, walimfuata.Public Domain Swahili New Testament -- PLEASE MAKE COPIES FOR YOUR FRIENDS, NO ROYALTY DUE.

Bible Hub

Matthew 3
Top of Page
Top of Page