Matayo 3
Swahili NT
1Siku hizo Yohane Mbatizaji alitokea, akaanza kuhubiri katika jangwa la Yudea: 2Tubuni, maana Ufalme wa mbinguni umekaribia.

3Huyu Yohane ndiye yule ambaye nabii Isaya alinena juu yake aliposema: "Sauti ya mtu imesikika jangwani: Mtayarishieni Bwana njia yake, nyoosheni vijia vyake."

4Yohane alivaa vazi lililoshonwa kwa manyoya ya ngamia, na ukanda wa ngozi kiunoni mwake. Chakula chake kilikuwa nzige na asali ya mwituni. 5Basi, watu kutoka Yerusalemu, kutoka mkoa wote wa Yudea na sehemu zote za kandokando ya mto Yordani, walimwendea, 6wakaziungama dhambi zao, naye akawabatiza katika mto Yordani.

7Lakini alipowaona Mafarisayo wengi na Masadukayo wanamjia ili awabatize, aliwaambia, "Enyi kizazi cha nyoka! Ni nani aliyewadokezea kwamba mnaweza kuiepuka ghadhabu inayokuja? 8Onyesheni basi kwa matendo, kwamba mmetubu kweli. 9Msidhani kwamba mtaweza kujitetea kwa kusema, Baba yetu ni Abrahamu! Nawaambieni hakika, Mungu anaweza kuyafanya mawe haya yawe watoto wa Abrahamu. 10Basi, shoka liko tayari kuikata mizizi ya miti; hivyo, kila mti usiozaa matunda mazuri, utakatwa na kutupwa motoni.

11Mimi ninawabatizeni kwa maji kuonyesha kwamba mmetubu. Lakini yule anayekuja baada yangu ana uwezo kuliko mimi. Mimi sistahili hata kubeba viatu vyake. Yeye atawabatizeni kwa Roho Mtakatifu na kwa moto. 12Yeye anashika mkononi chombo cha kupuria nafaka, ili aipure nafaka yake; akusanye ngano ghalani, na makapi ayachome kwa moto usiozimika."

13Wakati huo Yesu alitoka Galilaya akafika katika mto Yordani, akamwendea Yohane ili abatizwe naye. 14Lakini Yohane alijaribu kumzuia akisema, "Je, wewe unakuja kwangu? Mimi hasa ndiye ninayehitaji kubatizwa nawe." 15Lakini Yesu akamjibu, "Acha tu iwe hivyo kwa sasa, maana kwa namna hii inafaa tuyatekeleze yale yote Mungu anayotaka." Hapo Yohane akakubali. 16Mara tu Yesu alipokwisha batizwa, alitoka majini; na ghafla mbingu zikafunguka, akaona Roho wa Mungu akishuka kama njiwa na kutua juu yake. 17Sauti kutoka mbinguni ikasema, "Huyu ndiye Mwanangu mpendwa, nimependezwa naye."Public Domain Swahili New Testament -- PLEASE MAKE COPIES FOR YOUR FRIENDS, NO ROYALTY DUE.

Bible Hub

Matthew 2
Top of Page
Top of Page