Luka 13
Swahili NT
1Wakati huo watu fulani walikuja, wakamweleza Yesu juu ya watu wa Galilaya ambao Pilato alikuwa amewaua wakati walipokuwa wanachinja wanyama wao wa tambiko. 2Naye Yesu akawaambia, "Mnadhani Wagalilaya hao walikuwa wahalifu zaidi kuliko Wagalilaya wengine, ati kwa sababu wameteseka hivyo? 3Nawaambieni hakika sivyo; lakini nanyi, hali kadhalika, msipotubu, mtaangamia kama wao. 4Au wale kumi na wanane walioangukiwa na mnara kule Siloamu wakafa; mnadhani wao walikuwa wakosefu zaidi kuliko wengine wote walioishi Yerusalemu? 5Nawaambieni sivyo; lakini nanyi msipotubu, mtaangamia kama wao."

6Kisha, Yesu akawaambia mfano huu: "Mtu mmoja alikuwa na mtini katika shamba lake. Mtu huyu akaenda akitaka kuchuma matunda yake, lakini akaukuta haujazaa hata tunda moja. 7Basi, akamwambia mfanyakazi wake: Angalia! Kwa miaka mitatu nimekuwa nikija kuchuma matunda ya mtini huu, nami nisiambulie kitu. Ukate! Kwa nini uitumie ardhi bure? 8Lakini naye akamjibu: Bwana, tuuache tena mwaka huu; nitauzungushia mtaro na kuutilia mbolea. 9Kama ukizaa matunda mwaka ujao, vema; la sivyo, basi utaweza kuukata."

10Yesu alikuwa akifundisha katika sunagogi moja siku ya Sabato. 11Na hapo palikuwa na mwanamke mmoja aliyekuwa mgonjwa kwa miaka kumi na minane kutokana na pepo aliyekuwa amempagaa. Kwa sababu hiyo, mwili wake ulikuwa umepindika vibaya hata asiweze kusimama wima. 12Yesu alipomwona, alimwita, akamwambia, "Mama, umeponywa ugonjwa wako." 13Akamwekea mikono, na mara mwili wake ukawa wima tena, akawa anamtukuza Mungu. 14Lakini mkuu wa sunagogi alikasirika kwa sababu Yesu alikuwa amemponya siku ya Sabato. Hivyo akawaambia wale watu walikusanyika pale, "Mnazo siku sita za kufanya kazi. Basi, fikeni siku hizo mkaponywe magonjwa yenu; lakini msije siku ya Sabato." 15Hapo Bwana akamjibu, "Enyi wanafiki! Nani kati yenu hangemfungua ng'ombe au punda wake kutoka zizini ampeleke kunywa maji, hata kama siku hiyo ni ya Sabato? 16Sasa, hapa yupo binti wa Abrahamu ambaye Shetani alimfanya kilema kwa muda wa miaka kumi na minane. Je, haikuwa vizuri kumfungulia vifungo vyake siku ya Sabato?" 17Alipokwisha sema hayo, wapinzani wake waliona aibu lakini watu wengine wote wakajaa furaha kwa sababu ya mambo yote aliyotenda.

18Yesu akauliza: "Ufalme wa Mungu unafanana na nini? Nitaulinganisha na nini? 19NI kama mbegu ya haradali aliyotwaa mtu mmoja na kuipanda shambani mwake; ikaota hata ikawa mti. Ndege wa angani wakajenga viota vyao katika matawi yake."

20Tena akauliza: "Nitaulinganisha Ufalme wa Mungu na nini? 21Ni kama chachu aliyoitwaa mama mmoja na kuichanganya pamoja na unga debe moja kisha unga wote ukaumuka wote."

22Yesu alindelea na safari yake kwenda Yerusalemu huku akipitia mijini na vijijini, akihubiri. 23Mtu mmoja akamwuliza, "Je, Mwalimu, watu watakaookoka ni wachache?" 24Yesu akawaambia, "Jitahidini kuingia kwa kupitia mlango mwembamba; maana nawaambieni, wengi watajaribu kuingia lakini hawataweza. 25Wakati utakuja ambapo mwenye nyumba atainuka na kufunga mlango. Ninyi mtasimama nje na kuanza kupiga hodi mkisema: Bwana, tufungulie mlango. Lakini yeye atawajibu: Sijui mmetoka wapi. 26Nanyi mtaanza kumwambia: Sisi ndio wale tuliokula na kunywa pamoja nawe; na wewe ulifundisha katika vijiji vyetu. 27Lakini yeye atasema: Sijui ninyi mmetoka wapi; ondokeni mbele yangu, enyi nyote watenda maovu. 28Ndipo mtakuwa na kulia na kusaga meno, wakati mtakapowaona Abrahamu, Isaka na Yakobo, na manabii wote wapo katika Ufalme wa Mungu, lakini ninyi wenyewe mmetupwa nje! 29Watu watakuja kutoka mashariki na magharibi, kutoka kaskazini na kusini, watakuja na kukaa kwenye karamu katika Ufalme wa Mungu. 30Naam, wale walio wa mwisho watakuwa wa kwanza; na wale walio wa kwanza watakuwa wa mwisho."

31Wakati huohuo, Mafarisayo na watu wengine walimwendea Yesu wakamwambia, "Ondoka hapa uende mahali pengine, kwa maana Herode anataka kukuua." 32Yesu akawajibu, "Nendeni mkamwambie huyo mbweha hivi: Leo na kesho ninafukuza pepo na kuponya wagonjwa, na siku ya tatu nitakamilisha kazi yangu. 33Hata hivyo, kwa leo, kesho na kesho kutwa, ni lazima niendelee na safari yangu, kwa sababu si sawa nabii auawe nje ya Yerusalemu. 34Yerusalemu! We Yerusalemu! Unawaua manabii na kuwapiga mawe wale waliotumwa kwako! Mara ngapi nimetaka kuwakusanya watoto wako pamoja kama kuku anavyokusanya vifaranga vyake chini ya mabawa yake, Lakini wewe umekataa. 35Haya, utaachiwa mwenyewe nyumba yako. Naam, hakika nawaambieni, hamtaniona mpaka wakati utakapofika mseme: Abarikiwe huyo ajaye kwa jina la Bwana."



Public Domain Swahili New Testament -- PLEASE MAKE COPIES FOR YOUR FRIENDS, NO ROYALTY DUE.

Bible Hub

Luke 12
Top of Page
Top of Page