Swahili NT 1Msiwahukumu wengine, msije nanyi mkahukumiwa na Mungu;
2kwa maana jinsi mnavyowahukumu wengine, ndivyo nanyi mtakavyohukumiwa; na kipimo kilekile mnachotumia kwa wengine ndicho Mungu atakachotumia kwenu.
3Kwa nini wakiona kibanzi kilicho jichoni mwa ndugu yako, na papo hapo huioni boriti iliyoko jichoni mwako?
4Au, wawezaje kumwambia ndugu yako, Ndugu, ngoja nikuondoe kibanzi jichoni mwako, wakati wewe mwenyewe unayo boriti jichoni mwako?
5Mnafiki wewe! Ondoa kwanza boriti iliyoko jichoni mwako na hapo ndipo utaona waziwazi kiasi cha kuweza kuondoa kibanzi kilichoko jichoni mwa ndugu yako. 6Msiwape mbwa vitu vitakatifu wasije wakageuka na kuwararua ninyi; wala msiwatupie nguruwe lulu zenu wasije wakazikanyaga. 7Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtapata; bisheni, nanyi mtafunguliwa. 8Maana, aombaye hupewa, atafutaye hupata, na abishaye hufunguliwa. 9Je, kuna yeyote miongoni mwenu ambaye mtoto wake akimwomba mkate, atampa jiwe? 10Au je, akimwomba samaki, atampa nyoka? 11Kama basi ninyi, ingawa ni waovu, mwajua kuwapa watoto wenu vitu vizuri, hakika Baba yenu wa mbinguni atafanya zaidi: atawapa mema wale wanaomwomba. 12Watendeeni wengine yale mnayotaka wao wawatendee ninyi. Hii ndiyo maana ya Sheria ya Mose na mafundisho ya manabii. 13Ingieni kwa kupitia mlango mwembamba. Kwa maana njia inayoongoza kwenye maangamizi ni pana, na mlango wa kuingilia humo ni mpana; waendao njia hiyo ni wengi. 14Lakini njia inayoongoza kwenye uzima ni nyembamba, na mlango wa kuingilia humo ni mwembamba; ni watu wachache tu wanaoweza kuigundua njia hiyo. 15Jihadharini na manabii wa uongo. Wao huja kwenu wakionekana kama kondoo kwa nje, lakini kwa ndani ni mbwa mwitu wakali. 16Mtawatambua kwa matendo yao. Je, watu huchuma zabibu katika miti ya miiba, au tini katika mbigili? La! 17Basi, mti mwema huzaa matunda mema, na mti mbaya huzaa matunda mabaya. 18Mti mwema hauwezi kuzaa matunda mabaya, wala mti mbaya hauwezi kuzaa matunda mema. 19Kila mti usiozaa matunda mema utakatwa na kutupwa motoni. 20Kwa hiyo, mtawatambua kwa matendo yao. 21Si kila aniambiaye, Bwana, Bwana, ataingia katika Ufalme wa mbinguni; ila ni yule tu anayetimiza mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni. 22Wengi wataniambia Siku ile ya hukumu: Bwana, Bwana! kwa jina lako tulitangaza ujumbe wako, na kwa jina lako tuliwatoa pepo na kufanya miujiza mingi. 23Hapo nitawaambia: Sikuwajua ninyi kamwe; ondokeni mbele yangu, enyi watenda maovu. 24Kwa sababu hiyo, kila mtu anayeyasikia maneno yangu na kuyazingatia, anafanana na mtu mwenye busara, aliyejenga nyumba yake juu ya mwamba. 25Mvua ikanyesha, mito ikafurika, pepo kali zikavuma na kuipiga nyumba hiyo. Lakini haikuanguka kwa sababu ilikuwa imejengwa juu ya mwamba. 26Lakini yeyote anayesikia maneno yangu haya bila kuyazingatia, anafanana na mtu mpumbavu aliyejenga nyumba yake juu ya mchanga. 27Mvua ikanyesha, mito ikafurika, pepo kali zikavuma na kuipiga nyumba hiyo, nayo ikaanguka; tena kwa kishindo kikubwa." 28Yesu alipomaliza kusema maneno hayo, umati wa watu ukashangazwa na mafundisho yake. 29Hakuwa kama walimu wao wa Sheria, bali alifundisha kwa mamlaka. Public Domain Swahili New Testament -- PLEASE MAKE COPIES FOR YOUR FRIENDS, NO ROYALTY DUE. Bible Hub |