Luka 6
Swahili NT
1Siku moja ya Sabato, Yesu alikuwa anapita katika mashamba ya ngano, na wanafunzi wake wakaanza kukwanyua masuke ya ngano, wakaondoa punje zake kwa mikono, wakala. 2Baadhi ya Mafarisayo wakawauliza, "Mbona mnafanya jambo ambalo si halali siku ya Sabato?" 3Yesu akawajibu, "Je, hamjasoma jinsi alivyofanya Daudi pamoja na wenzake wakati walipokuwa na njaa? 4Yeye aliingia ndani ya nyumba ya Mungu, akachukua ile mikate iliyowekwa mbele ya Mungu, akala na kuwapa wenzake. Kisheria, ni makuhani tu peke yao ndio walioruhusiwa kula mikate hiyo." 5Hivyo akawaambia, "Mwana wa Mtu ni Bwana wa Sabato."

6Siku nyingine ya Sabato, Yesu aliingia katika sunagogi, akafundisha. Mle ndani mlikuwa na mtu ambaye mkono wake wa kuume ulikuwa umepooza. 7Walimu wa Sheria na Mafarisayo walitaka kupata kisingizio cha kumshtaki Yesu na hivyo wakawa wanangojea waone kama angemponya mtu siku ya Sabato. 8Lakini Yesu alijua mawazo yao, akamwambia yule mwenye mkono uliopooza, "Inuka, simama katikati." Yule mtu akaenda akasimama katikati. 9Kisha Yesu akawaambia, "Nawaulizeni, je, ni halali siku ya Sabato kutenda jambo jema au kutenda jambo baya; kuokoa maisha au kuyaangamiza?" 10Baada ya kuwatazama wote waliokuwa pale, akamwambia yule mtu, "Nyosha mkono wako." Naye akafanya hivyo, na mkono wake ukawa mzima tena. 11Lakini wao wakakasirika sana, wakajadiliana jinsi ya kumtendea Yesu maovu.

12Siku moja Yesu alikwenda mlimani kusali, akakesha huko usiku kucha akimwomba Mungu. 13Kesho yake aliwaita wanafunzi wake, na miongoni mwao akachagua kumi na wawili ambao aliwaita mitume: 14Simoni (ambaye Yesu alimpa jina Petro) na Andrea ndugu yake, Yakobo na Yohane, Filipo na Bartholomayo, 15Mathayo na Thoma, Yakobo wa Alfayo na Simoni (aliyeitwa Zelote), 16Yuda wa Yakobo na Yuda Iskarioti ambaye baadaye alikuwa msaliti.

17Baada ya kushuka mlimani pamoja na mitume, Yesu alisimama mahali palipokuwa tambarare. Hapo palikuwa na kundi kubwa la wanafunzi wake na umati wa watu waliotoka pande zote za Yudea na Yerusalemu na pwani ya Tiro na Sidoni. Wote walifika kumsikiliza Yesu na kuponywa magonjwa yao. 18Aliwaponya pia wote waliokuwa wanasumbuliwa na pepo wachafu. 19Watu wote walitaka kumgusa, kwa maana nguvu ilikuwa inatoka ndani yake na kuwaponya wote.

20Yesu akawageukia wanafunzi wake, akasema: "Heri ninyi mlio maskini, maana Ufalme wa Mungu ni wenu. 21Heri ninyi mnaosikia njaa sasa, maana baadaye mtashiba. Heri ninyi mnaolia sasa, maana baadaye mtacheka kwa furaha. 22Heri yenu ninyi iwapo watu watawachukia, watawatenga, watawatukana na kuwaharibieni jina kwa ajili ya Mwana wa Mtu! 23Wakati hayo yatakapotokea, furahini na kucheza, maana hakika tuzo lenu ni kubwa mbinguni. Kwa maana wazee wao waliwatendea manabii vivyo hivyo. 24Lakini ole wenu ninyi mlio matajiri, maana mmekwisha pata faraja yenu. 25Ole wenu ninyi mnaoshiba sasa, maana baadaye mtasikia njaa. Ole wenu ninyi mnaocheka kwa furaha sasa, maana baadaye mtaomboleza na kulia. 26Ole wenu ninyi iwapo watu wote wanawasifu, maana wazee wao waliwafanyia manabii wa uongo vivyo hivyo.

27Lakini nawaambieni ninyi mnaonisikiliza: wapendeni adui zenu, watendeeni mema wale wanaowachukieni. 28Watakieni baraka wale wanaowalaani, na waombeeni wale wanaowatendea vibaya. 29Mtu akikupiga shavu moja mgeuzie na la pili. Mtu akikunyang'anya koti lako mwachie pia shati lako. 30Yeyote anayekuomba mpe, na mtu akikunyang'anya mali yako usimtake akurudishie. 31Watendeeni wengine kama mnavyotaka wawatendee ninyi. 32Na ikiwa mnawapenda tu wale wanaowapenda ninyi, je, mtapata tuzo gani? Hakuna! Kwa maana hata wenye dhambi huwapenda wale wanaowapenda wao. 33Tena, kama mkiwatendea mema wale tu wanaowatendeeni mema, mtapata tuzo gani? Hata wenye dhambi hufanya vivyo hivyo! 34Na kama mnawakopesha wale tu mnaotumaini watawalipeni, je, mtapata tuzo gani? Hata wenye dhambi huwakopesha wenye dhambi wenzao ili warudishiwe kima kilekile! 35Ila nyinyi wapendeni adui zenu, na kuwatendea mema; kopesheni bila kutazamia malipo, na tuzo lenu litakuwa kubwa, nanyi mtakuwa watoto wa Mungu aliye juu. Kwa maana yeye ni mwema kwa wale wasio na shukrani na walio wabaya. 36Muwe na huruma kama Baba yenu alivyo na huruma.

37Msiwahukumu wengine, nanyi hamtahukumiwa; msiwalaumu wengine, nanyi hamtalaumiwa; wasameheni wengine, nanyi mtasamehewa. 38Wapeni wengine wanavyohitaji, nanyi mtapewa. Naam, mtapokea mikononi mwenu kipimo kilichojaa, kikashindiliwa na kusukwasukwa hata kumwagika. Kwa maana kipimo kilekile mnachotumia kwa wengine ndicho ambacho Mungu atatumia kwenu."

39Akawaambia mfano huu: "Je, kipofu anaweza kumwongoza kipofu mwenzake? La! Wote wataanguka shimoni. 40Mwanafunzi hamshindi mwalimu wake, lakini kila mwanafunzi akisha hitimu huwa kama mwalimu wake. 41Unawezaje kukiona kibanzi kilicho katika jicho la mwenzio, usione boriti iliyo katika jicho lako mwenyewe? 42Au, unawezaje kumwambia mwenzako, Ndugu, ngoja nikuondoe kibanzi katika jicho lako, na huku huioni boriti iliyoko katika jicho lako mwenyewe? Mnafiki wewe! Toa kwanza boriti iliyoko jichoni mwako, na hivyo utaona sawasawa kiasi cha kuweza kuondoa kibanzi kilicho katika jicho la ndugu yako. 43Mti mwema hauzai matunda mabaya, wala mti mbaya hauzai matunda mazuri. 44Watu huutambua mti kutokana na matunda yake. Ni wazi kwamba watu hawachumi tini katika michongoma, wala hawachumi zabibu katika mbigili. 45Mtu mwema hutoa yaliyo mema kutoka katika hazina bora iliyo moyoni mwake; na mtu mbaya hutoa yaliyo mabaya katika hazina mbaya iliyo moyoni mwake, kwa maana mtu huongea kutokana na yale yaliyojaa moyoni mwake.

46Mbona mwaniita Bwana, Bwana, na huku hamtimizi yale ninayosema? 47Nitawapeni mfano unaofaa kuonyesha alivyo yeyote yule anayekuja kwangu, akasikia maneno yangu na kuyatimiza: 48Huyo anafanana na mtu ajengaye nyumba, ambaye amechimba chini na kuweka msingi wake juu ya mwamba; kukatokea mafuriko ya mto, mkondo wa maji ukaipiga nyumba ile, lakini haukuweza kuitikisa, kwa sababu ilikuwa imejengwa imara. 49Lakini yeyote anayesikia maneno yangu lakini asifanye chochote, huyo anafanana na mtu aliyejenga nyumba juu ya udongo, bila msingi. Mafuriko ya mto yakatokea, mkondo wa maji ukaipiga nyumba ile, ikaanguka na kuharibika kabisa!"



Public Domain Swahili New Testament -- PLEASE MAKE COPIES FOR YOUR FRIENDS, NO ROYALTY DUE.

Bible Hub

Luke 5
Top of Page
Top of Page