Wakolosai 1
Swahili NT
1Mimi Paulo, mtume wa Kristo Yesu kwa mapenzi ya Mungu, na ndugu Timotheo,

2tunawaandikia ninyi watu wa Mungu huko Kolosai, ndugu zetu waaminifu katika kuungana na Kristo. Tunawatakieni neema na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu.

3Daima tunamshukuru Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, wakati tunapowaombea. 4Maana tumesikia juu ya imani yenu katika Kristo Yesu na juu ya upendo wenu kwa watu wote wa Mungu. 5Wakati ujumbe ule wa kweli, yaani Habari Njema, ilipowafikieni kwa mara ya kwanza, mlipata kusikia juu ya lile tumaini linalopatikana kwake. Kwa sababu hiyo imani na upendo wenu vinategemea jambo lile mnalotumainia ambalo mmewekewa salama mbinguni. 6Habari Njema inazidi kuzaa matunda na kuenea ulimwenguni kote kama vile ilivyofanya kwenu ninyi tangu siku ile mliposikia juu ya neema ya Mungu na kuitambua ilivyo kweli. 7Mlijifunza juu ya neema ya Mungu kutoka kwa Epafra, mtumishi mwenzetu, ambaye ni mfanyakazi mwaminifu wa Kristo kwa niaba yetu. 8Yeye alitupa habari za upendo wenu mliojaliwa na Roho.

9Kwa sababu hiyo tumekuwa tukiwaombeeni daima tangu tulipopata habari zenu. Tunamwomba Mungu awajazeni ujuzi kamili wa mapenzi yake, awajazeni hekima yote na elimu iletwayo na Roho wake. 10Hapo mtaweza kuishi kama anavyotaka Bwana na kutenda daima yanayompendeza. Maisha yenu yatakuwa yenye matunda ya kila namna ya matendo mema na mtazidi kukua katika kumjua Mungu. 11Mungu awajalieni nguvu kwa uwezo wake mtukufu ili mweze kustahimili kila kitu kwa uvumilivu. 12Na kwa furaha, mshukuruni Baba aliyewawezesha ninyi kuwa na sehemu yenu katika mambo yale Mungu aliyowawekea watu wake katika utawala wa mwanga.

13Yeye alituokoa katika nguvu ya giza, akatuleta salama katika ufalme wa Mwanae mpenzi, 14ambaye kwa njia yake tunakombolewa, yaani dhambi zetu zinaondolewa.

15Kristo ni mfano wa Mungu asiyeonekana; ni mzaliwa wa kwanza wa viumbe vyote. 16Maana kwa njia yake vitu vyote viliumbwa duniani na mbinguni, vitu vinavyoonekana na visivyoonekana: wenye enzi, watawala, wakuu na wenye mamlaka. Vyote viliumbwa kwa njia yake na kwa ajili yake. 17Kristo alikuwako kabla ya vitu vyote; kwa kuungana naye, vyote vyadumu mahali pake. 18Yeye ni kichwa cha mwili wake, yaani kanisa; yeye ni chanzo cha uhai wa huo mwili. Yeye ndiye mwanzo, mzaliwa wa kwanza aliyefufuliwa kutoka wafu, ili awe na nafasi ya kwanza katika vitu vyote. 19Maana Mungu alipenda utimilifu wote uwe ndani yake. 20Kwa njia yake Mungu alivipatanisha naye vitu vyote naam, viumbe vyote mbinguni na duniania; alileta amani kwa damu ya Kristo msalabani.

21Hapo kwanza ninyi pia mlikuwa mbali na Mungu na mlikuwa adui zake kwa sababu ya fikira zenu na matendo yenu maovu. 22Lakini sasa, kwa kifo cha Mwanae aliyeishi hapa duniani, Mungu amewapatanisha naye, kusudi awalete mbele yake mkiwa watakatifu, safi na bila lawama. 23Mnapaswa, lakini kuendelea kuwa imara na thabiti katika imani hiyo, na msikubali kusukumwa mbali na tumaini lile mlilopata wakati mlipoisikia Habari Njema. Mimi Paulo nimekuwa mtumishi wa hiyo Habari Njema ambayo imekwisha hubiriwa kila kiumbe duniani.

24Na sasa nafurahi kuteseka kwa ajili yenu, maana kwa mateso yangu hapa duniani, nasaidia kukamilisha kile kilichopungua bado katika mateso ya Kristo kwa ajili ya mwili wake, yaani kanisa. 25Nami nimefanywa kuwa mtumishi wa kanisa kufuatana na mpango wake Mungu ambao alinikabidhi kwa faida yenu. Mpango wenyewe ni kuutangaza kwa ukamilifu ujumbe wake, 26ambao ni siri aliyowaficha binadamu wote tangu milele, lakini sasa amewajulisha watu wake. 27Mpango wa Mungu ni kuwajulisha watu wake siri hii kuu na tukufu ambayo ni kwa ajili ya watu wote. Na, siri yenyewe ndiyo hii: Kristo yuko ndani yenu, na jambo hilo lamaanisha kwamba ninyi mtaushiriki utukufu wa Mungu. 28Kwa sababu hiyo tunamhubiri Kristo kwa watu wote; tunawaonya na kuwafundisha wote kwa hekima yote, ili tuweze kumleta kila mmoja mbele ya Mungu akiwa amekomaa katika kuungana na Kristo. 29Kwa madhumuni hayo mimi nafanya kazi na kujitahidi nikiitumia nguvu kuu ya Kristo ifanyayo kazi ndani yangu.Public Domain Swahili New Testament -- PLEASE MAKE COPIES FOR YOUR FRIENDS, NO ROYALTY DUE.

Bible Hub

Philippians 4
Top of Page
Top of Page