Matayo 11
Swahili NT
1Yesu alipomaliza kuwapa wanafunzi kumi na wawili maagizo, alitoka hapo, akaenda kufundisha na kuhubiri katika miji yao.

2Yohane mbatizaji akiwa gerezani alipata habari juu ya matendo ya Kristo. Basi, Yohane akawatuma wanafunzi wake, 3wamwulize: "Je, wewe ni yule anayekuja, au tumngoje mwingine?" 4Yesu akawajibu, "Nendeni mkamwambie Yohane mambo mnayoyasikia na kuyaona: 5vipofu wanaona, viwete wanatembea, wenye ukoma wanatakaswa na viziwi wanasikia, wafu wanafufuliwa na maskini wanahubiriwa Habari Njema. 6Heri mtu yule asiyekuwa na mashaka nami."

7Basi, hao wajumbe wa Yohane walipokuwa wanakwenda zao, Yesu alianza kuyaambia makundi ya watu habari za Yohane: "Mlikwenda kutazama nini kule jangwani? Je, mlitaka kuona mwanzi unaotikiswa na upepo? 8Lakini mlikwenda kuona nini? Mlikwenda kumtazama mtu aliyevaa mavazi maridadi? Watu wanaovaa mavazi maridadi hukaa katika nyumba za wafalme. 9Basi, mlikwenda kuona nini? Nabii? Naam, hakika ni zaidi ya nabii.

10Huyu ndiye anayesemwa katika Maandiko Matakatifu: Tazama, hapa namtuma mjumbe wangu, asema Bwana, akutangulie na kukutayarishia njia yako.

11Kweli nawaambieni, miongoni mwa watoto wote wa watu, hajatokea aliye mkuu kuliko Yohane mbatizaji. Hata hivyo, yule aliye mdogo kabisa katika Ufalme wa mbinguni, ni mkubwa kuliko yeye. 12Tangu wakati wa Yohane mbatizaji mpaka leo hii, Ufalme wa mbinguni unashambuliwa vikali, na watu wakali wanajaribu kuunyakua kwa nguvu. 13Mafundisho yote ya manabii na sheria yalibashiri juu ya nyakati hizi. 14Kama mwaweza kukubali basi, Yohane ndiye Eliya ambaye angekuja. 15Mwenye masikio na asikie!

16Basi, nitakifananisha kizazi hiki na kitu gani? Ni kama vijana waliokuwa wamekaa uwanjani, wakawa wakiambiana kikundi kimoja kwa kingine: 17Tumewapigieni ngoma lakini hamkucheza; tumeimba nyimbo za huzuni lakini hamkulia! 18Kwa maana Yohane alikuja, akafunga na wala hakunywa divai, nao wakasema: Amepagawa na pepo. 19Mwana wa Mtu akaja, anakula na kunywa, nao wakasema: Mtazameni huyu, mlafi na mlevi, rafiki yao watoza ushuru na wahalifu! Hata hivyo, hekima ya Mungu inathibitishwa kuwa njema kutokana na matendo yake."

20Kisha Yesu akaanza kuilaumu miji ambayo, ingawaje alifanya miujiza mingi humo, watu wake hawakutaka kubadili nia zao mbaya: 21Ole wako Korazini! Ole wako Bethsaida! Maana, kama miujiza iliyofanyika kwako ingalifanyika kule Tiro na Sidoni, watu wake wangalikwisha vaa mavazi ya gunia na kujipaka majivu zamani, ili kuonyesha kwamba wametubu. 22Hata hivyo nawaambieni, Siku ya hukumu, ninyi mtapata adhabu kubwa kuliko Tiro na Sidoni. 23Na wewe Kafarnaumu, je, utajikweza mpaka mbinguni? Utaporomoshwa mpaka Kuzimu! Maana, kama miujiza iliyofanyika kwako ingalifanyika kule Sodoma, mji huo ungalikuwako mpaka hivi leo. 24Lakini nawaambieni, Siku ya hukumu itakuwa nafuu zaidi kwa watu wa Sodoma, kuliko kwako wewe."

25Wakati huo Yesu alisema, "Nakushukuru ee Baba, Bwana wa mbingu na dunia, maana umewaficha wenye hekima mambo haya, ukawafumbulia watoto wadogo. 26Naam Baba, ndivyo ilivyokupendeza. 27Baba yangu amenikabidhi vitu vyote. Hakuna amjuaye Mwana ila Baba, wala amjuaye Baba ila Mwana, na yeyote yule ambaye Mwana atapenda kumjulisha.

28Njoni kwangu ninyi nyote msumbukao na kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. 29Jifungeni nira yangu, mkajifunze kwangu, maana mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo, nanyi mtatulizwa rohoni mwenu. 30Maana, nira niwapayo mimi ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi."



Public Domain Swahili New Testament -- PLEASE MAKE COPIES FOR YOUR FRIENDS, NO ROYALTY DUE.

Bible Hub

Matthew 10
Top of Page
Top of Page