3 Yohana 1
Swahili NT
1Mimi mzee nakuandikia wewe Gayo, rafiki yangu, ninayekupenda kweli.

2Mpenzi wangu, nakutakia mafanikio mema ya kila aina; nakutakia afya njema ya mwili kama ulivyo nayo rohoni. 3Nimefurahi sana ndugu kadhaa walipofika hapa, wakaiambia juu ya uaminifu wako kuhusu ukweli; naam, wewe unaishi daima katika ukweli. 4Hakuna kitu kinachonifurahisha zaidi kuliko kusikia kwamba watoto wangu wanaishi katika ukweli.

5Mpenzi wangu, wewe ni mwaminifu kila mara unapowahudumia ndugu, hata kama ni wageni. 6Ndugu hao wamelieleza kanisa hapa habari za upendo wako. Tafadhali uwasaidie waendelee na safari yao kwa namna itakayompendeza Mungu, 7Maana wanaanza safari yao katika utumishi wa Kristo bila kupokea msaada wowote kutoka kwa watu wasioamini. 8Basi, sisi tunapaswa kuwasaidia watu hawa, ili nasi tupate kushiriki katika kazi yao kwa ajili ya ukweli.

9Niliandika barua fupi kwa hilo kanisa; lakini Diotrefe, ambaye hupenda kuwa kiongozi wao, hataki kabisa kunisikiliza. 10Basi, nitakapokuja nitayafichua mambo yote anayofanya, maneno mabaya anayotutolea na uongo anaosema juu yetu. Isitoshe, yeye hukataa kuwakaribisha hao ndugu walio safarini, na hata huwazuia watu wengine wanaotaka kuwakaribisha, na hujaribu kuwafukuzia nje ya kanisa.

11Mpenzi wangu, usifuate mfano mbaya, bali mfano mwema. Kila atendaye mema ni wa Mungu; lakini anayetenda mabaya hajapata kumwona Mungu. 12Kila mtu anamsifu Demetrio; naam, ukweli wenyewe unamsifu. Nasi pia tunatoa ushahidi wetu juu yake, nawe wajua kwamba tunachosema ni kweli.

13Ninayo bado mengi ya kukwambia, lakini sipendi kuyaandika kwa kalamu na wino.

14Natumaini kukuona karibuni na hapo tutazungumza ana kwa ana. (G1-15) Nakutakia amani. Rafiki zako wanakusalimu. Wasalimu rafiki zetu wote kila mmoja binafsi.Public Domain Swahili New Testament -- PLEASE MAKE COPIES FOR YOUR FRIENDS, NO ROYALTY DUE.

Bible Hub

2 John 1
Top of Page
Top of Page