2 Petro 1
Swahili NT
1Mimi Simoni Petro, mtumishi na mtume wa Yesu Kristo, nawaandikia ninyi ambao, kwa wema wake Mungu wetu, na Mwokozi Yesu Kristo, mmejaliwa imani ileile ya thamani kuu tuliyojaliwa sisi. 2Nawatakieni neema na amani tele katika kumjua Mungu na Yesu Bwana wetu. 3Kwa uwezo wake wa kimungu, Mungu ametujalia mambo yote tunayohitaji, ili tuishi maisha ya kumcha Mungu kwa kumjua yeye aliyetuita tuushiriki utukufu na wema wake yeye mwenyewe. 4Kwa namna hiyo ametujalia zawadi kuu na za thamani ambazo alituahidia, ili kwa zawadi hizo mpate kuziepa kabisa tamaa mbaya zilizomo duniani, na mpate kuishiriki hali yake ya kimungu. 5Kwa sababu hiyo, fanyeni bidii ya kuongeza fadhila katika imani yenu: ongezeni elimu katika fadhila yenu, 6kuwa na kiasi katika elimu yenu, uvumilivu katika kuwa na kiasi, uchaji wa Mungu katika uvumilivu wenu, 7udugu katika uchaji wenu, na mapendo katika udugu wenu. 8Mkiwa na sifa hizo zote kwa wingi, zitawawezesheni kuwa watendaji na kupata faida katika kumjua Bwana wetu Yesu Kristo. 9Lakini mtu asiye na sifa hizo ni kipofu, hawezi kuona na amesahau kwamba alikwisha takaswa dhambi zake za zamani. 10Kwa hiyo basi, ndugu zangu, fanyeni bidii zaidi kuufanya huo wito wenu mlioitiwa na Mungu uwe jambo la kudumu katika maisha yenu; kama mkiishi namna hiyo hamtaanguka kamwe. 11Kwa namna hiyo mtafaulu kupewa haki kamili ya kuingia katika Utawala wa milele wa Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo.

12Kwa hiyo nitaendelea kuwakumbusheni daima mambo haya, ingawa mmekwisha yafahamu, na mko imara katika ukweli mlioupokea. 13Nadhani ni jambo jema kwangu, muda wote niishio hapa duniani, kuwapeni moyo na kuwakumbusheni juu ya mambo haya. 14Najua kwamba karibu nitauweka kando mwili huu wenye kufa, kama Bwana alivyoniambia waziwazi. 15Basi, nitajitahidi kuwapatieni njia ya kuyakumbuka mambo haya kila wakati, baada ya kufariki kwangu.

16Wakati tulipowafundisheni juu ya ukuu wa kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo, hatukutegemea hadithi tupu zisizo na msingi. Sisi tuliuona utukufu wake kwa macho yetu wenyewe. 17Sisi tulikuwapo wakati alipopewa heshima na kutukuzwa na Mungu Baba, wakati sauti ilipomjia kutoka kwake yeye aliye Utukufu Mkuu, ikisema: "Huyu ni Mwanangu mpenzi, nimependezwa naye." 18Tena, sisi wenyewe tulisikia sauti hiyo kutoka mbinguni wakati tulipokuwa pamoja naye juu ya ule mlima mtakatifu.

19Tena, ujumbe wa manabii watuthibitishia jambo hilo; nanyi mwafanya vema kama mkiuzingatia, maana ni kama taa inayoangaza mahali penye giza mpaka Siku ile itakapopambazuka na mwanga wa nyota ya asubuhi utakapong'ara mioyoni mwenu. 20Zaidi ya hayo, lakini, kumbukeni kwamba hakuna mtu yeyote awezaye kufafanua mwenyewe unabii ulio katika Maandiko Matakatifu. 21Maana hakuna ujumbe wa kinabii unaotokana na matakwa ya binadamu, bali watu walinena ujumbe wa Mungu wakiongozwa na Roho Mtakatifu.Public Domain Swahili New Testament -- PLEASE MAKE COPIES FOR YOUR FRIENDS, NO ROYALTY DUE.

Bible Hub

1 Peter 5
Top of Page
Top of Page