Swahili NT 1Mungu alituahidia kwamba tutaweza kupata pumziko hilo alilosema. Basi, na tuogope ili yeyote kati yenu asije akashindwa kupata pumziko hilo.
2Maana Habari Njema imehubiriwa kwetu kama vile ilivyohubiriwa kwa hao watu wa kale. Lakini ujumbe huo haukuwafaa chochote, maana waliusikia lakini hawakuupokea kwa imani. 3Basi, sisi tunaoamini tunapata pumziko hilo aliloahidi Mungu. Kama alivyosema: "Nilikasirika, nikaapa: Hawataingia huko ambako ningewapa pumziko." Mungu alisema hayo ingawa kazi yake ilikuwa imekwisha malizika tangu alipoumba ulimwengu. 4Maana Maandiko yasema mahali fulani kuhusu siku ya saba: "Mungu alipumzika siku ya saba, akaacha kazi zake zote." 5Tena jambo hili lasemwa pia: "Hawataingia huko ambako ningewapa pumziko." 6Wale waliotangulia kuhubiriwa Habari Njema hawakupata pumziko hilo kwa sababu hawakuamini. Wapo, basi, wengine ambao wangejaliwa kulipata. 7Jambo hili ni wazi, kwani Mungu aliweka siku nyingine ambayo inaitwa "Leo". Miaka mingi baadaye Mungu alisema juu ya hiyo siku kwa maneno ya Daudi katika Maandiko yaliyokwisha tajwa: "Kama mkisikia sauti ya Mungu leo, msiifanye mioyo yenu kuwa migumu." 8Kama Yoshua angaliwapa watu hao hilo pumziko, Mungu hangalisema baadaye juu ya siku nyingine. 9Kwa hiyo, basi, bado lipo pumziko kwa watu wa Mungu kama kule kupumzika kwake Mungu siku ya saba. 10Maana, kila anayepata pumziko aliloahidi Mungu atapumzika baada ya kazi yake kama vile pia Mungu alivyopumzika baada ya yake. 11Basi, tujitahidi kupata pumziko hilo, ili asiwepo yeyote miongoni mwenu atakayeshindwa, kama walivyofanya wao kwa sababu ya ukosefu wao wa imani. 12Neno la Mungu ni hai na lina nguvu; ni kali zaidi kuliko upanga wenye makali kuwili. Hukata kabisa mpaka mahali ambapo moyo na roho hukutana, mpaka pale vikutanapo viungo vya mwili na mafuta. Neno hilo huchambua nia na fikira za mioyo ya watu. 13Hakuna kiumbe chochote kilichofichika mbele ya Mungu; kila kitu kimefunuliwa wazi mbele ya macho yake. Kwake, sisi sote tutapaswa kutoa hoja ya matendo yetu. 14Basi, tunapaswa kuzingatia kwa uthabiti imani tunayoiungama. Maana tunaye Kuhani Mkuu aliyeingia mpaka kwa Mungu mwenyewe--Yesu, Mwana wa Mungu. 15Huyu Kuhani Mkuu wetu si mmoja ambaye hawezi kutuunga mkono katika unyonge wetu, ila ni Kuhani Mkuu ambaye alijaribiwa kama sisi kwa kila namna lakini hakutenda dhambi. 16Basi, na tukikaribie bila hofu kiti cha enzi cha Mungu, palipo na neema, ili tukajipatie huruma na neema ya kutusaidia wakati wa lazima. Public Domain Swahili New Testament -- PLEASE MAKE COPIES FOR YOUR FRIENDS, NO ROYALTY DUE. Bible Hub |