2 Wakorintho 10
Swahili NT
1Mimi Paulo mwenyewe ambaye naonekana kuwa mpole nikiwa pamoja nanyi, lakini mkali wakati nikiwa mbali nanyi, nawasihini kwa huruma na wema wake Kristo. 2Nawaombeni msinisababishe kuwa mkali wakati nitakapokuja, maana nina hakika naweza kuwa mkali kwa wote wale wanaotudhania kwamba tunaishi kidunia. 3Kweli tunaishi duniani, lakini hatupigani vita kidunia. 4Maana, silaha tunazotumia katika vita vyetu si silaha za kidunia, ila ni nguvu za Mungu zenye kuharibu ngome zote. Tunaharibu hoja zote za uongo, 5na kubomoa kila kizuizi cha majivuno kilichowekwa kuipinga elimu ya Mungu; tunaziteka fikira zote na kuzifanya zimtii Kristo. 6Mkisha kuwa wakamilifu katika kutii, sisi tuko tayari kuadhibu kila namna ya kutotii.

7Ninyi hutazama mambo kwa nje tu. Je, yupo mtu yeyote anayedhani kwamba yeye ni wa Kristo? Sawa! Basi, afikirie vilevile kwamba sisi pia ni wa Kristo kama yeye alivyo wa Kristo. 8Hata kama nimezidi katika kujivuna kwangu juu ya ule uwezo aliotupa--uwezo wa kuwajenga na sio wa kubomoa--hata hivyo sijutii hata kidogo. 9Sipendi mfikiri kwamba nataka kuwatisha ninyi kwa barua zangu. 10Mtu anaweza kusema: "Barua za Paulo ni kali na zenye maneno mazito, lakini yeye mwenyewe anapokuwa pamoja nasi ni mtu dhaifu, na hata anapoongea maneno yake ni kama si kitu." 11Mtu asemaye hivyo heri akumbuke kwamba hakuna tofauti ya yale tunayoandika katika barua wakati tuko mbali, na yale tutakayofanya wakati tutakapokuwa nanyi.

12Kwa vyovyote hatungethubutu kujiweka au kujilinganisha na wale watu wanaojisifia wenyewe. Watu wenye kujifanya wao kuwa kipimo cha kujipimia, na watu wanaojilinganisha wenyewe kwa wenyewe, ni wapumbavu. 13Lakini sisi hatutajivuna kupita kiasi; kujivuna huko kutabaki katika kile kipimo cha kazi aliyotukabidhi Mungu, kazi ambayo tunaifanya pia kwenu. 14Na kwa vile ninyi mu katika mipaka hiyo, hatukuipita tulipokuja kwenu, tukiwaleteeni Habari Njema juu ya Kristo. 15Basi, hatujivunii kazi waliyofanya wengine zaidi ya kipimo tulichopewa; ila tunatumaini kwamba imani yenu itazidi miongoni mwenu kufuatana na kipimo alichotuwekea Mungu. 16Hapo tutaweza kuihubiri Habari Njema katika nchi nyingine, mbali nanyi; na haitakuwa shauri la kujivunia kazi waliyofanya watu wengine mahali pengine. 17Lakini kama yasemavyo Maandiko: "Mwenye kuona fahari na aone fahari juu ya alichofanya Bwana." 18Anayekubaliwa si yule anayejisifu mwenyewe, bali yule anayesifiwa na Bwana.



Public Domain Swahili New Testament -- PLEASE MAKE COPIES FOR YOUR FRIENDS, NO ROYALTY DUE.

Bible Hub

2 Corinthians 9
Top of Page
Top of Page