Ufunua was Yohana 16
Swahili NT
1Kisha nikasikia sauti kubwa kutoka Hekaluni ikiwaambia wale malaika saba, "Nendeni mkamwage mabakuli hayo saba ya ghadhabu ya Mungu duniani."

2Basi, malaika wa kwanza akaenda akamwaga bakuli lake juu ya nchi. Mara madonda mabaya na ya kuumiza sana yakawapata wote waliokuwa na alama ya yule mnyama, na wale walioiabudu sanamu yake.

3Kisha malaika wa pili akamwaga bakuli lake baharini. Nayo bahari ikawa damu tupu kama damu ya mtu aliyekufa, na viumbe vyote hai baharini vikafa.

4Malaika wa tatu akamwaga bakuli lake katika mito na chemchemi za maji, navyo vikageuka damu. 5Nikamsikia malaika msimamizi wa maji akisema, "Ewe mtakatifu, Uliyeko na uliyekuwako! Wewe ni mwenye haki katika hukumu hii uliyotoa. 6Maana waliimwaga damu ya watu wako na ya manabii, nawe umewapa damu wainywe; wamestahili hivyo!" 7Kisha nikasikia sauti madhabahuni ikisema, "Naam, Bwana Mungu Mwenye Uwezo! Hukumu zako ni za kweli na haki!"

8Kisha malaika wa nne akamwaga bakuli lake juu ya jua. Jua likapewa nguvu ya kuwachoma watu kwa moto wake. 9Basi, watu wakaunguzwa vibaya sana; wakamtukana Mungu aliye na uwezo juu ya mabaa hayo makubwa. Lakini hawakuziacha dhambi zao na kumtukuza Mungu.

10Kisha malaika wa tano akamwaga bakuli lake juu ya makao makuu ya yule mnyama. Giza likauvamia utawala wake, watu wakauma ndimi zao kwa sababu za maumivu, 11wakamtukana Mungu wa mbinguni kwa sababu ya maumivu yao na madonda yao. Lakini hawakuyaacha matendo yao mabaya.

12Kisha malaika wa sita akamwaga bakuli lake juu ya mto mkubwa uitwao Eufrate. Maji yake yakakauka, na hivyo njia ilitengenezwa kwa ajili ya wafalme wa mashariki.

13Kisha nikaona pepo wabaya watatu walio kama vyura, wakitoka kinywani mwa yule joka, kinywani mwa yule mnyama, na kinywani mwa yule nabii wa uongo. 14Hawa ndio roho za pepo wafanyao miujiza. Ndio wanaokwenda kwa wafalme wa ulimwengu wote na kuwakusanya pamoja kwa ajili ya vita kuu Siku ile ya Mungu Mwenye Uwezo. 15Sikiliza! Mimi naja kama mwizi! Heri mtu akeshaye na kuvaa nguo zake ili asije akaenda uchi huko na huko mbele ya watu. 16Basi, roho hao wakawakusanya hao wafalme mahali paitwapo kwa Kiebrania Harmagedoni.

17Kisha malaika wa saba akamwaga bakuli lake hewani. Sauti kubwa ikasikika kutoka kwenye kiti cha enzi, Hekaluni, ikisema, "Mwisho umefika!" 18Kukatokea umeme, kelele, ngurumo na tetemeko kubwa la ardhi ambalo halijapata kutokea tangu Mungu alipomuumba mtu. 19Mji ule mkuu ukapasuliwa sehemu tatu, nayo miji ya mataifa ikateketea. Babuloni, mji mkuu, haukusahauliwa na Mungu. Aliunywesha kikombe cha divai ya ghadhabu yake kuu. 20Visiwa vyote vikatoweka, nayo milima haikuonekena tena. 21Mvua ya mawe makubwa yenye uzito wa kama kilo hamsini kila moja, ikawanyeshea watu. Nao wakamtukana Mungu kwa sababu ya mapigo ya mvua hiyo ya mawe. Naam, pigo la mvua hiyo ya mawe lilikuwa kubwa mno.Public Domain Swahili New Testament -- PLEASE MAKE COPIES FOR YOUR FRIENDS, NO ROYALTY DUE.

Bible Hub

Revelation 15
Top of Page
Top of Page