Yakobo 1
Swahili NT
1Mimi Yakobo, mtumishi wa Mungu na wa Bwana Yesu Kristo, nawaandikia ninyi, makabila kumi na mawili, yaliyotawanyika ulimwenguni! Salaam!

2Ndugu zangu, muwe na furaha mnapopatwa na majaribu mbalimbali, 3kwani mwajua kwamba imani yenu ikisha stahimili, itawapatieni uvumilivu. 4Muwe na hakika kwamba uvumilivu wenu utawategemeza mpaka mwisho, mpate kuwa wakamilifu na watimilifu, bila kupungukiwa chochote.

5Lakini kama mmoja wenu ametindikiwa hekima, basi, anapaswa kumwomba Mungu ambaye atampatia; kwani Mungu huwapa wote kwa wingi na kwa ukarimu. 6Lakini anapaswa kuomba kwa imani bila mashaka yoyote. Mtu aliye na mashaka ni kama mawimbi ya bahari ambayo husukumwa na kutupwatupwa na upepo. 7Mtu wa namna hiyo, mwenye nia mbili na asiye na msimamo katika mwenendo wake wote, 8asidhani ya kwamba atapata chochote kile kutoka kwa Bwana.

9Ndugu aliye maskini anapaswa kufurahi wakati Mungu anapomkweza, 10naye tajiri anapaswa kufurahi anaposhushwa na Mungu. Maana tajiri atatoweka kama ua la porini. 11Jua huchomoza na kwa joto lake kali hukausha mimea, nayo maua yake huanguka, na uzuri wake wote huharibika. Vivyo hivyo, tajiri ataangamizwa katika shughuli zake.

12Heri mtu anayebaki mwaminifu katika majaribu, kwani akisha stahimili atapewa tuzo la uzima ambalo Mungu aliwaahidia wale wanaompenda. 13Kama mtu akijaribiwa, asiseme: "Ninajaribiwa na Mungu." Maana Mungu hawezi kujaribiwa na uovu, wala yeye hamjaribu mtu yeyote. 14Lakini mtu hujaribiwa anapovutwa na kunaswa na tamaa zake mbaya. 15Tamaa ikiiva huzaa dhambi; nayo dhambi ikikomaa huzaa kifo. 16Ndugu zangu wapenzi, msidanganyike! 17Kila kipaji chema na kila zawadi kamilifu hutoka mbinguni; hutoka kwa Baba, Muumba wa mianga, ambaye habadiliki wala hana alama yoyote ya ugeugeu. 18Kwa kupenda kwake mwenyewe alituzaa kwa neno lake la ukweli, ili tuwe namna ya matunda ya kwanza miongoni mwa viumbe vyake.

19Ndugu zangu wapenzi, kumbukeni jambo hili! Kila mtu na awe mwepesi wa kusikia lakini asiwe mwepesi wa kusema wala mwepesi wa kukasirika. 20Mwenye hasira hawezi kutimiza matakwa ya Mungu yaliyo ya haki. 21Kwa hiyo, tupilieni mbali mwenendo mchafu na tabia zote mbovu; jiwekeni chini ya Mungu na kupokea ule ujumbe uliopandwa mioyoni mwenu, ambao waweza kuziokoa nafsi zenu. 22Msijidanganye wenyewe kwa kusikiliza tu neno lake, bali litekelezeni kwa vitendo. 23Yeyote anayesikiliza hilo neno lakini halitekelezi, huyo ni kama mtu anayejiangalia sura yake mwenyewe katika kioo. 24Hujiangalia mwenyewe, kisha huenda zake, na mara husahau jinsi alivyo. 25Lakini mtu anayeangalia kwa makini sheria kamilifu ambayo huwapa watu uhuru, mtu anayeendelea kuizingatia, na si kuisikia tu na kuisahau baadaye, bali anaitekeleza, mtu huyo atabarikiwa katika kila kitu anachofanya.

26Kama mtu akijiona kuwa ni mtu mwenye dini, lakini hawezi kuutawala ulimi wake, dini yake haifai kitu, na anajidanganya mwenyewe. 27Dini iliyo safi na isiyo na hitilafu mbele ya Mungu Baba ni hii: Kuwasaidia yatima na wajane katika shida zao, na kujilinda mwenyewe usichafuliwe na ulimwengu huu.



Public Domain Swahili New Testament -- PLEASE MAKE COPIES FOR YOUR FRIENDS, NO ROYALTY DUE.

Bible Hub

Hebrews 13
Top of Page
Top of Page