Waebrania 1
Swahili NT
1Hapo zamani, Mungu alisema na babu zetu mara nyingi kwa namna nyingi kwa njia ya manabii, 2lakini siku hizi za mwisho, amesema nasi kwa njia ya Mwanae. Yeye ndiye ambaye kwa njia yake Mungu aliumba ulimwengu na akamteua avimiliki vitu vyote. 3Yeye ni mng'ao wa utukufu wa Mungu, na mfano kamili wa hali ya Mungu mwenyewe, akiutegemeza ulimwengu kwa neno lake lenye nguvu. Baada ya kuwapatia binadamu msamaha wa dhambi zao, aliketi huko juu mbinguni, upande wa kulia wa Mungu Mkuu. 4Mwana ni mkuu zaidi kuliko malaika, kama vile jina alilopewa na Mungu ni kuu zaidi kuliko jina lao.

5Maana Mungu hakumwambia kamwe hata mmoja wa malaika wake: "Wewe ni Mwanangu; Mimi leo nimekuwa Baba yako." Wala hakusema juu ya malaika yeyote: "Mimi nitakuwa Baba yake, naye atakuwa Mwanangu."

6Lakini Mungu alipokuwa anamtuma Mwanae mzaliwa wa kwanza ulimwenguni, alisema: "Malaika wote wa Mungu wanapaswa kumwabudu."

7Lakini kuhusu malaika, Mungu alisema: "Mungu awafanya malaika wake kuwa pepo, na watumishi wake kuwa ndimi za moto."

8Lakini kumhusu Mwana, Mungu alisema: "Utawala wako ee Mungu, wadumu milele na milele! Wewe wawatawala watu wako kwa haki.

9Wewe wapenda uadilifu na kuchukia uovu. Ndiyo maana Mungu, Mungu wako amekuweka wakfu na kukumiminia furaha kubwa zaidi kuliko wenzako."

10Pia alisema: "Bwana, wewe uliumba dunia hapo mwanzo, mbingu ni kazi ya mikono yako.

11Hizo zitatoweka, lakini wewe wabaki daima, zote zitachakaa kama vazi.

12Utazikunjakunja kama koti, nazo zitabadilishwa kama vazi. Lakini wewe ni yuleyule daima, na maisha yako hayatakoma."

13Mungu hakumwambia kamwe hata mmoja wa malaika wake: "Keti upande wangu wa kulia, mpaka niwaweke adui zako chini ya miguu yako."

14Malaika ni roho tu wanaomtumikia Mungu, na Mungu huwatuma wawasaidie wale watakaopokea wokovu.Public Domain Swahili New Testament -- PLEASE MAKE COPIES FOR YOUR FRIENDS, NO ROYALTY DUE.

Bible Hub

Philemon 1
Top of Page
Top of Page